Kinana aitwa Dodoma, Membe afukuzwa

11Jul 2020
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Kinana aitwa Dodoma, Membe afukuzwa

HALMASHAURI Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), imemsamehe Katibu Mkuu mstaafu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana, na kumwondolea vizuizi alivyowekewa awali, huku ikibariki kufukuzwa uanachama kwa Benard Membe.

Kikao hicho kilifanyika jana chini ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais John Magufuli, kikihudhuriwa na wajumbe 166.

Akizungumza katika kikao hicho, Dk. Magufuli alisema Februari, mwaka huu, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, ilitoa adhabu kwa baadhi ya wanachama ambao walikiuka maadili na misingi ya chama.

“Nimeona nilichomeke hapahapa kwa kuwa ndiyo kikao cha uamuzi. Kwa hiyo, wajumbe wenzangu wa kamati kuu mnisamehe sana, lakini kubwa ni kwamba kikao kile kilitoa mapendekezo ya adhabu kwa baadhi ya wanachama wetu kutokana na misingi halali ya chama chetu.

"Lakini, hivi karibuni kama miezi minne mitano, mwenzetu mmoja ambaye ni Katibu Mkuu mstaafu (Kinana) alijitokeza hadharani kule Arusha na shahidi ni Mwenyekiti wa CCM Arusha, akaomba radhi, akajutia kwa kitendo alichofanya, kikubwa zaidi ndugu yetu aliomba radhi hadharani, ni kitendo ambacho ni kigumu watu wa kawaida kukifanya," alisema.

Dk. Magufuli alisema kitendo hicho kinahitaji nguvu ya Mungu kutubu hadharani, akibainisha kuwa aliguswa kwa kiwango kikubwa na kitendo hicho cha Kinana.

“Nina uhakika na ninyi wajumbe mliguswa sana, alikuwa amepewa adhabu ya miezi 18 na kalipio, na hakukataa kutumikia adhabu ile na hadi sasa ameshatumikia miezi kati ya minne au mitano.

"Niliona wajumbe wa NEC, chama chenye huruma na mapenzi mema, chama dume, niwaombe kama itawezekana kwa huruma yenu huyu ndugu yetu ambaye amekubali kutumikia adhabu yake hadi sasa tumsamehe," aliomba.

Kutokana na kauli hiyo, wajumbe wa kikao hicho walisikika wakisema "amesamehewa".

"Yule mwingine ambaye sitaki kumtaja, jina yeye ameshaondoka moja kwa moja, kwa hiyo adhabu ile si mnaikubali ya kumfukuza?” Dk. Magufuli aliuliza.

Aliwahoji wajumbe kuhusu hoja hiyo ambayo waliitikia "ndiyo" kuashiria kwamba wanakubaliana na uamuzi wa kumfukuza uanachama wa CCM aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Membe.

Wakati wa kuhitimisha hoja hiyo, Dk. Magufuli alitangaza kuwa Kinana amesamehewa rasmi kupitia kikao hicho na kumtaka ashirikiane na wana CCM kuchapa kazi huku akisisitiza CCM ni chama chenye huruma, upendo, kuzingatia maadili na miiko na kipo kwa ajili ya kuwatumikia Watanzania.

Dk. Magufuli pia alimkaribisha Kinana Dodoma ili ashiriki vikao vya juu vya uamuzi vya chama hicho vinavyoendelea leo jijini hapa.

Habari Kubwa