Kinara mtihani kidato cha nne alivyopokewa kifalme Mbeya

23Jan 2021
Nebart Msokwa
MBEYA
Nipashe
Kinara mtihani kidato cha nne alivyopokewa kifalme Mbeya

MWANAFUNZI Paul Luziga (17), aliyeongoza kitaifa katika matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha nne mwaka jana, amepata mapokezi ya kifalme alipowasili shuleni Panda Hill katika Bonde la Songwe mkoani Mbeya.

Kinara wa matokeo ya mtihani wa Kidato cha Nne 2020, Paul Luziga, akipunga mkono juu ya gari wakati alipopokelewa na msururu wa magari baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe (SIA), jijini Mbeya jana, akielekea shuleni Panda Hill kwa ajili ya kupongezwa na walimu pamoja na wanafunzi wa shule hiyo. PICHA: NEBART MSOKWA

Kinara huyo ambaye wakati wa matokeo yakitangazwa na Baraza la Mitihani (NECTA) alikuwa jijini Dar es Salaam, amelazimika kurejea mkoani Mbeya kwa ndege baada ya uongozi wa shule yake kumlipia tiketi ya usafiri huo ya kwenda na kurudi ili wampongeze.

Alipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe (SIA), mwanafunzi huyo alishuhudia maajabu baada ya kukuta magari zaidi ya 20 aina ya Coaster yakiwa yamewabeba wanafunzi wenzake zaidi ya 500 na walimu wao waliofika uwanjani huko kumlaki.

Umati huo wa wanafunzi ambao walibeba mabango yenye ujumbe wa kumpongeza mwamba huyo, ulisababisha baadhi ya wananchi nao kujongea uwanjani huko kushuhudia kinachoendelea.

Mwanafunzi kinara wa matokeo ya Kidato cha Nne 2020, Paul Luziga (kushoto) akipongezwa kwa kushikana mkono na Mkuu wa Shule ya Sekondari Panda Hill ya mkoani Mbeya juzi alipofika shuleni hapo kwa mwaliko wa uongozi wa shule hiyo kwa lengo la . PICHA NA NEBART MSOKWA.

Shughuli hiyo ilisababisha uwanja huo wa ndege kufurika watu waliohitaji kumwona na hata wasafiri wengine walilazimika kusubiri mpaka umati huo upungue ndipo waondoke.

Kwa mujibu wa taratibu za uwanja huo, ni wanafunzi wachache sana walioruhusiwa kuingia ndani ya jengo la kupokea abiria kumsubiri shujaa huyo, hivyo wengine walilazimika kumsubiria nje.

Luziga aliwasili uwanjani huko kwa ndege ya Shirika la Ndege la Taifa (ATCL) majira ya saa tisa alasiri na kulakiwa na wenyeji wake ambao walikuwa wamejipanga kwa namna ya kipekee kwa ajili ya tukio hilo.

SUTI MAALUM

Wakati kinara huyo anapokewa, baadhi ya wanafunzi waliandaliwa kwa kushonewa suti maalum zenye rangi nyeusi na miwani ya rangi nyeusi zilizowafanya waonekane kama walinzi wa Rais.

Baada ya kushuka kwenye ndege, Luziga alivishwa taji maalum na wanafunzi wenzake lililokuwa na maandishi yaliyosomeka ‘Paul Luziga, Tanzania One (T.O) 2020’ na kupewa maua maalum kisha akapandishwa kwenye gari maalum lenye paa la wazi tayari kwa safari ya kuelekea shuleni.

Mwanafunzi kinara wa matokeo ya Kidato cha Nne 2020, Paul Luziga (aliyevaa taji na maua) akinyoosha mkono kuashiria ushindi wakati alipokuwa anasalimiana na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Panda Hill aliyosoma alipowasili shuleni hapo kupongezwa na walimu, kulia kwake ni mama yake mzazi, Lucy Mogela. PICHA NA NEBART MSOKWA.

Baada ya kupanda kwenye gari huku akipunga mkono na kukunja ngumi kuashiria ushindi, gari lilianza safari, huku likiwa limezungukwa na ‘walinzi’ hao ambao walikuwa wananing’inia kwenye milango mpaka msafara ulipofika Barabara Kuu ya Tanzania na Zambia (TANZAM).

Msafara huo uliokuwa na magari zaidi ya 20 yakiongozwa na gari la Polisi aina ya Probox, ambalo lilitangulia na kuzuia magari yote katika Barabara Kuu kupisha msafara huo, ulianza safari kuelekea shuleni.

Kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa, msafara huo ulielekea katikati ya Mji Mdogo wa Mbalizi ulioko takriban kilometa 10 kutoka uwanjani huko na kuzunguka barabara kadhaa za mji huo kabla ya kurejea shuleni umbali wa zaidi ya kilomita 20.

KAULI YA MKUU WA SHULE

Akitoa historia ya kitaaluma ya Luziga, Mkuu wa Shule ya Panda Hill, Zephania Lusanika, alisema kijana huyo alikuwa anafanya vizuri tangu kwenye mtihani wa usaili mwaka 2016 ambapo alishika nafasi ya tatu kati ya wanafunzi 800 waliofanya mtihani huo kwa kupata wastani wa 92.

Alisema kijana huyo alidhihirisha zaidi ubora wake kwenye Mtihani wa Kidato cha Pili Mwaka 2018 ambapo alifanya vizuri zaidi kuliko wenzake na kuwa wa kwanza.

Alisema kwenye mtihani wa kujipima wa kidato cha nne, kijana huyo alifaulu kwa kupata daraja la kwanza la alama nane (8), lakini kwenye mtihani wa jimbo, aliongeza juhudi na kupata daraja la kwanza la alama saba (7).

Alisema kuwa kabla ya kufanya mtihani wa taifa, kijana huyo aliwaahidi walimu wake kuwa angefaulu, lakini siyo kwa kiwango ambacho amefikia cha kuwa kinara kitaifa.

“Aliwaahidi walimu wake kuwa atafanya vizuri kwenye mitihani yake na kuwapeleka bungeni jijini Dodoma badala ya Mlimani City jijini Dar es Salaam. Kwa hiyo, tulikuwa tunajua atafanya vizuri ila siyo kwa kiwango hicho,” alisema Lusanika.

Alisema shule hiyo ina wanafunzi wengi na wanafanya vizuri kwa sababu wanalelewa katika mazingira ya kujituma, kuwa na nidhamu na kumtumikia Mungu.

Alisema katika miaka 10 iliyopita shule hiyo imekuwa ikifanya vizuri na imekuwa miongoni mwa shule 50 bora kitaifa, huku wanafunzi wakijitokeza kwenye orodha ya vinara 10 kwenye matokeo ya kidato cha nne na cha sita.

MAMA WA SHUJAA

Mama mzazi wa Luziga, Lucy Mogela, alisema alipokea matokeo ya mwanawe huyo kwa mshtuko uliosababisha adondoshe machozi ya furaha kila anapopigiwa simu na watu kumpongeza kuhusu matokeo ya mwanawe.

Alisema Paul ni mtoto wake wa mwisho kuzaliwa kati ya watoto sita na kwamba wote wamesoma, lakini hakuna aliyefaulu kwa kiwango cha juu kama kijana huyo.

Mama huyo ambaye ni mjane, alisema mwanawe huyo alianza kuonyesha kuwa ana akili nyingi wakati akiwa mdogo ambapo alikuwa anahoji maswali mengi ambayo yalikuwa yanaashiria kuwa na upeo mkubwa.

“Kila mzazi anayempeleka mtoto wake shuleni, huwa anatamani mtoto wake afanye vizuri, kwa hiyo mimi nimejawa na furaha kubwa sana na ninaamini ni mpango wa Mungu uliomwezesha mwanangu huyu,” alisema Lucy.

Aliwashukuru walimu na walezi wa wanafunzi wa shule hiyo kwa kumlea vyema mwanawe pamoja na wenzake na hivyo kuwafanya kufaulu vizuri kwenye mitihani yao huku akiwataka wanafunzi waliobaki, kumwamini Mungu.

SIRI YA MAFANIKIO

Akizungumza na wenzake baada ya kulakiwa shuleni huko huku akiwa amezingirwa na walinzi wake, Luziga alisema siri ya kufanya vizuri kwenye mitihani hiyo ni kujituma kwenye masomo na kumtumainia Mungu.

Alisema hata yeye hakutarajia kuwa angefaulu kwa kiwango hicho cha kuwa kinara kitaifa na hivyo matokeo hayo yalimshtua na hakuamini kabisa mwanzoni.

“Ninatamani sana kuwa injinia na ninaamini kuwa nitaweza, ninachoamini ni kwamba siri ya mafanikio yangu ni kujituma pamoja na kumtumainia Mungu, hivyo ninachowashauri wenzangu ni kuongeza bidii na kufuata kile wanachoelekezwa na walimu,” alisema Luziga.

Aliwashukuru walimu wake na wanafunzi wenzake kwa mapokezi aliyoyapata kuanzia uwanja wa ndege mpaka shuleni huko, akisisitiza kuwa ni historia kubwa kwenye maisha yake.

WANAFUNZI WALONGA

Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo, walisema matokeo ya Luziga yamekuwa ni changamoto kubwa kwao kwa kuwa yameiletea heshima shule yao ambayo hata wao wanatakiwa kuitetea watakapofanya mitihani.

Mmoja wa wanafunzi hao, Sued Ndanzi, ambaye ni mwanafunzi wa Kidato cha Nne, alisema ufaulu wa kijana huyo unawafanya na wao kuwa na wivu wa kutaka wafanye vizuri na kufanyiwa sherehe kama hiyo.

Alisema wanafunzi wengi huwa wanakuwa na uwezo, lakini wanashindwa kufanya vizuri kutokana na kutojituma kwenye masomo na kutozingatia kile wanachofundishwa.

“Walimu wetu wameamua kumfanyia mwenzetu kitu hiki ili kutuhamasisha sisi tuliobaki, wanatueleza kabisa kwamba kila mtu anaweza kuwa T.O (Tanzania One), hivyo tunaamini hii ni hamasa kwetu,” alisema Ndazi.

Elizabeth Mwalukana, mwanafunzi mwingine katika shule hiyo, alisema watahakikisha wanamtumia kijana huyo kama dira yao kwa kujituma zaidi kwenye mitihani ya kidato cha nne na cha sita ili kuiendeleza sifa ya shule hiyo.

Aliuomba uongozi wa shule hiyo kuendelea kuwafanyia sherehe wanafunzi wanaofanya vizuri, ili kuendelea kuweka hamasa kwa wanafunzi wa shule hiyo kuongeza juhudi.

Kuanzia katika Uwanja wa Ndege mpaka kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Panda Hill, wanafunzi walikuwa wanaimba wimbo wa kumpongeza kijana huyo wakisema ‘We T.O! we T.O! we T.O!’

Januari 15, mwaka huu, Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Charles Msonde, alitangaza matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne, Kidato cha Pili na Darasa la Nne na kubainisha kuwa Tanzania One kwa Kidato cha Nne ametoka katika shule hiyo ya mkoani Mbeya.

Habari Kubwa