Kiongozi Mwenge wa uhuru aridhishwa na miradi Shinyanga

11Jul 2021
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe Jumapili
Kiongozi Mwenge wa uhuru aridhishwa na miradi Shinyanga

KIONGOZI wa mbio za mwenge wa uhuru Kitaifa Luteni Josephine Mwambashi, ameweka mawe ya msingi na kuona miradi mbalimbali ya maendeleo Manispaa ya Shinyanga na wilaya ya Shinyanga, ambapo ameridhishwa na miradi hiyo, na hakuna ambao ameukataa.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa uhuru Luteni Josephine Mwambashi, akiweka jiwe la Msingi katika Jengo la uthibiti ubora Kanda ya Magharibi.

Zoezi la mbio maalum za Mwenge wa uhuru kitaifa wilayani Shinyanga na Manispaa ya Shinyanga, limefanyika leo mara baada ya Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Jonas Mkude, kuukabidhi kwa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko katika viwanja wa michezo Shule ya Secondari Mwalukwa wilayani humo.

Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Patrobas Katambi, ambaye pia ni Naibu Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, vijana na ajira, akishika mwenge wa uhuru.

Mwambashi akizungumza wakati wa ukaguzi wa miradi yote Sita, amesema ameridhishwa na miradi hiyo ambayo imeendana na thamani ya fedha (Value for Money), huku kukiwa na salio la fedha kwenye baadhi ya miradi, na kuagiza ile ambayo haijakamilika kujengwa ikamilishwe haraka ili ianze kutoa huduma.

“Nimekagua miradi yote iko vizuri, na nimeweka jiwe la msingi, na ile ambayo nimetoa maelekezo yafanyiwe kazi, pamoja na kuikamilisha ile ambayo bado ipo kwenye hatua ya ujenzi ili itoe huduma haraka kwa wananchi,” amesema Luteni Mwambashi.

Pia amewapongeza wananchi wa Bushushu kwa kujitoa kuchangia ujenzi wa Zahanati, ambayo itawasaidia kuondokana na adha ya kufuata huduma za matibabu umbari mrefu.

Koplo Rehema Ali Haji ambaye ni miongoni mwa viongozi wakimbiza mwenge wa uhuru, akimtwisha ndoo ya maji mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Patrobas Katambi, wakati mwenge wa uhuru ulipofika kuona maendeleo ya mradi wa maji Ziwa Victoria uliopo Masekelo ambao unatekelezwa na mamala ya maji mjini Shinyanga SHUWASA.

Aidha akizungumza wakati akitoa ujumbe wa Mwenge wa uhuru, amewataka Watanzania, kudumisha amani, kuendeleza mapambano ya Rushwa, madawa ya kulevya, virusi vya ukimwi, Malaria, kuzingatia lishe bora kwa watoto, pamoja na Halmashauri kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato kwa njia ya kieletronic.

Kwa upande wao Wabunge wa Shinyanga, akiwamo Mbunge wa Jimbo la Solwa Ahmed Salum, Patrobas Katambi Jimbo la Shinyanga mjini, pamoja na Christina Mzava wa vitimaalum, kwa nyakati tofauti waliahidi kuendelea kuwaletea maendeleo wananchi, pamoja na kukamilisha maboma yaliyosalia kujengwa.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, akisoma taarifa ya mbio za mwenge wa uhuru wilayani humo, amesema utakimbizwa Kilomita 136, pamoja na kukagua miradi Sita yenye gharama ya Sh. milioni 855.

Mbunge wa Jimbo la Solwa Ahmed Salum, akishika mwenge wa uhuru mara baada ya kuwasili wilayani Shinyanga Tayari kwa kukimbizwa .

Katika hatua Nyingine Mboneko amewashukuru wananchi wa Shinyanga, kujitokeza kwa wingi kwenye mbio hizo za Mwenge wa uhuru, huku akiwataka kuendelea kushirikiana na Serikali kwenye shughuli mbalimbali za maendeleo.

Kauli mbiu ya mwenge wa uhuru mwaka huu 2021 inasema “Tehama ni msingi wa Taifa endelevu, Itumike kwa usahihi na uwajibikaji.

Habari Kubwa