kipaumbele bosi mpya Tanesco hiki

09Jan 2017
Gwamaka Alipipi
Dar es Salaam
Nipashe
kipaumbele bosi mpya Tanesco hiki

SIKU saba baada ya kuteuliwa kuliongoza Shirika la Umeme Tanzani (Tanesco), Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Dk. Tito Mwinuka, amesema udhibiti upotevu wa mapato na ndiyo njia pekee ya kulifanya shirika hilo liwe na fedha za kutosha.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Dk. Tito Mwinuka.

Alisema jambo lingine muhimu linalopaswa kuzingatiwa ni kupata thamani halisi ya fedha katika matumizi yote ya shirika.

Januari 2, mwaka huu Rais John Magufuli alimteua Dk. Mwinuka kukaimu nafasi hiyo, baada ya kutengua uteuzi wa aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Felchesmi Mramba.

Kabla ya uteuzi huo, Dk. Mwinuka alikuwa ni mhadhiri na Mkuu wa Idara ya Mekanika na Uhandisi na Teknolojia (CoET) cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Dk. Mwinuka aliiambia Nipashe kuwa Tanesco inakabiliwa na changamoto mbalimbali yakiwamo ya madeni ya ambayo inayadai na inayodaiwa, bei ya umeme kupungua na changamoto ya miundombinu ya umeme.

“Changamoto ulizotaja ni za kweli. Zote zinahusiana na utendaji wa siku hadi siku,” alisema Dk. Mwinuka wakati akijibu moja ya maswali ya gazeti hili kupitia barua pepe.

Alipoulizwa Watanzania watarajie nini pamoja na mikakati aliyonayo ya kiutendaji ambayo anatarajia kuianzisha ili Tanesco liwe shirika linaloiletea faida kubwa Serikali, Dk. Mwinuka alisema kuwa lengo la muhimu kwa Tanesco ni kuwa na umeme wa kutosha kwa sasa na baadaye na vile vile Shirika kuwa na fedha za kutosha ili kutimiza majukumu yake.

Dk. Mwinuka aliongeza kuwa ni muhimu kusimamia miundombinu ya nchi vikiwamo vinu vya kuzalisha umeme ili viweze kuzalisha katika ufanisi wa juu.

“Hivyo basi ni muhimu kusimamia miundombinu yetu vikiwamo vinu vya kuzalisha umeme ili viweze kuzalisha katika ufanisi wa juu.

Na hii itahusisha mpangilio mzuri wa ukarabati pamoja na uwapo wa vipuri kwa muda muafaka. Ili shirika kuwa na pesa ni muhimu kudhibiti upotevu wa namna yoyote ile na vile vile kupata thamani ya pesa ‘value for money’ katika matumizi yetu yote,” alisema Dk. Mwinuka.

Juzi, Dk. Mwinuka alikaririwa na gazeti dada la The Guardian, juu ya mtihani mzito unaomkabili katika kutumikia nafasi aliyoteuliwa, lakini aliahidi kufanya kila awezalo kuhakikisha kuwa hawaangushi Watanzania wala Rais Magufuli.

Habari Kubwa