Kipenga urais, ubunge Chadema chapulizwa

30Jun 2020
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Kipenga urais, ubunge Chadema chapulizwa
  • *Mpeperusha bendera urais kujulikana Julai 29

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetangaza mchakato wa uchukuaji fomu za urais, ubunge na udiwani upande wa Tanzania Bara.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CHADEMA, Reginald Munisi, picha mtandao

Kimesema mchakato huo unatarajiwa kuanza rasmi Julai 4 mwaka huu kwa wagombea urais kuanza kuchukua, kujaza na kutafuta wadhamini hadi Julai 19 mwaka huu.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CHADEMA, Reginald Munisi, alitangaza kuanza kwa mchakato huo alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.

Alisema kuanzia Julai 4, yaani Jumamosi, wagombea urais wataanza kuchukua fomu za kuwania nafasi mbalimbali wao wenyewe au kutuma mawakala wao katika ofisi ya Katibu Mkuu Bara.

Alisema kila mgombea atakuwa na nafasi ya kujaza fomu na kutafuta udhamini katika kanda 10 zikiwamo nane za Tanzania Bara na mbili za Zanzibar.

“Kwenye kila kanda, mgombea anatakiwa kupata wadhamini wasiopungua 100 na kutakuwa na maofisa wa chama watakaokuwa wanawapatia maelekezo ya namna ya kujaza fomu hizo,” alisema.

Kuhusu mdhamini, Munisi alisema hatakiwi kuwa mjumbe wa mkutano mkuu wa CHADEMA ambao ndiyo utapitisha jina la mgombea katika hatua za mwisho za mchakato huo.

Munisi alisema Julai 19, itakuwa mwisho wa kuchukua fomu, kujaza, kutafuta wadhamini na kuzirejesha makao makuu ya chama.

Alisema Julai 22, Katibu Mkuu wa CHADEMA atawasilisha taarifa za watia nia katika mkutano wa kamati kuu ili ipendekeze wanaofaa kuingia katika hatua inayofuata.

Munisi alisema kuwa Julai 28, Baraza Kuu litakaa na kuchuja majina na baada ya hapo yatachekechwa na kupelekwa mkutano mkuu ambao utakaa Julai 29 na kupitisha jina la mgombea urais.

WABUNGE

Kuhusu mchakato wa wagombea nafasi ya ubunge, Munisi alisema fomu zitaanza kutolewa Julai 4 katika ofisi za majimbo na zitapatikana pia kwenye tovuti ya chama.

“Wagombea wote wanapaswa kuchukua fomu, kuzijaza na kuzirejesha kwa jimbo wanalogombea au wilaya kwa hatua zinazofuata na mwisho utakuwa Julai 10 saa 10:00 jioni," alisema.

Munisi alisema baada ya hapo hatua mbili zitafuata katika majimbo ikiwamo wagombea wote kuitwa na kamati za utendaji za jimbo na kuwahoji kuhusu sifa zao, uanachama wao, uadilifu wao na maono yao na watatoa alama kwa njia ya kujaza fomu.

Alisema hatua ya pili wataangalia kuhusu kukubalika kwa mtia nia husika katika nafasi ya ubunge, lakini hawataruhusiwa kukata jina kwa kuwa majina yote yataenda kwenye kura za maoni katika mkutano mkuu wa jimbo.

Alisema kura za maoni zitatoa mwelekeo wa nani anafaa kupeperusha bendera ya chama na baada ya kikao hicho, kamati ya utendaji itakaa tena kupendekeza na kufanya uteuzi wa awali.

“Watafanya mapendekezo ya awali ya nani ateuliwe kupeperusha bendera ya chama na mchakato wote huu utasimamiwa na uongozi wa kanda,” alisema.

Munisi alisema kuwa baada ya hapo, kamati ya utendaji ya kanda itakaa na kutoa maoni ya kwa kila mgombea na watawasilisha taarifa kwa Katibu Mkuu wa Chadema ambaye atawasilisha taarifa kwa kamati kuu ya chama ambayo itapitia mapendekezo yote na kuteua mgombea.

"Julai 30 hadi 31, kamati kuu itakaa kwa ajili ya kupitisha majina ya wagombea wa nafasi hizo katika majimbo yote nchini," alibainisha.

MADIWANI

Kuhusu mchakato wa madiwani, Munisi alisema fomu zitapatikana katika ofisi za kata, majimbo na tovuti ya chama.

Alisema kuanzia Julai 11 hadi 17 ni muda wa kuchukua na kurudisha fomu za kuwania nafasi ya udiwani na hatua nyingine zitafuta ikiwamo kuhojiwa na kamati ya utendaji ya kata ambayo itawapatia maksi.

Baada ya hapo watapigiwa kura ya maoni na kamati ya utendaji ya kata kuanzia Julai 20 hadi 23.

“Hizi zinachelewa kidogo ili mtu akiona nafasi ya ubunge haijaenda vizuri, aweze kuomba udiwani ili tusijepoteza watu ambao wana uwezo mzuri tu, anaweza asitoshe kwenye ubunge akatosha kwenye udiwani,” alifafanua.

Munisi aliongeza kuwa Julai 24, kamati ya utendaji za majimbo yote nchini, zitateua majina ya madiwani wa kupeperusha bendera ya CHADEMA.

VITI MAALUM

Kuhusu mchakato wa viti maalum, Munisi alisema uko kwenye mwongozo wa Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA) na ratiba yao iko kama ya wagombea wa majimbo.

Alisema wakati mkutano mkuu wa chama kanda ukipiga kura za maoni za wagombea, BAWACHA nao watapiga kura za maoni za viti maalum.

Alisema hadi kufika Septemba 25, watakuwa washapitisha majina ya Viti Maalum wa CHADEMA.

“Niwakumbushe Watanzania wote umuhimu wa zoezi tunaloenda kulifanya, maana ya uhuru, maana ya kujitawala ni kuweza kuamua ni nani sisi tunamtaka na siyo mtu mwingine atuamulie,” alisema.

Aliwakaribisha wanachama wote wa CHADEMA wenye sifa na nia ya kuwania nafasi mbalimbali kupitia Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, kujitokeza kuchukua fomu kuwania nafasi hizo.

Habari Kubwa