Kipindupindu chashika kasi Dodoma

27Feb 2016
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Kipindupindu chashika kasi Dodoma

MLIPUKO wa ugonjwa wa kipindupindu umeibuka kwa kasi mkoani Dodoma katika wilaya za Chamwino na Mpwapwa, ambapo wagonjwa zaidi ya 48 wameripotiwa katika vijiji vya Chipogolo, Loje na Uyenzele katika siku nne za mwezi huu.

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu.

Akizungumza na Nipashe juzi, Kaimu Mganga mkuu wa mkoa wa Dodoma, Dk. Nassoro Mzee, alisema ugonjwa huo ambao ulikuwa umepotea katika mkoa wa Dodoma, umerudi kwa kasi katika wilaya hizo ambazo idadi kubwa ya wagonjwa imeripotiwa kwa kipindi kifupi.
Wagonjwa 48 hao waliripotiwa kati ya Februari 16-20.

Dk. Mzee alisema Chamwino haikuwa na mgonjwa hata mmoja tangu Januari 19, mwaka huu na Mpwapwa haikuwa na mgonjwa tangu Agosti mwaka jana wakati ugonjwa huo ulipolipuka katika wilaya tano za mkoa wa Dodoma.

Katika wilaya ya Chamwino, alisema wagonjwa 25 waliripotiwa ndani ya siku mbili.

“Mpwapwa pia watu 23 wameripotiwa kuugua kipindupindu lakini idadi hii ya wagonjwa ni kuanzia tarehe 16 mwezi huu wa pili hadi tarehe 20,” alisema Dk. Mzee.

Alisema wamepeleka timu ya wataalamu wa afya kwenda kufanya tathimini na kuona namna wanavyoweza kuukabili kabla hali haijawa mbaya zaidi.

“Tulikwenda kuona nini mikakati ya hawa wenzetu wa halmashauri lakini pia tumepeleka vifaa mbalimbali kama vile dripu pamoja na sindano," alisena na kubainisha "katika wilaya hizi mbili tumetoa dripu 190, Chamwino 120 na Mpwapwa 70.”

Aliongeza kuwa katika kukabiliana na ugonjwa huo wameshauriana na wakurugenzi wa halmashauri hizo kuweka mikakati madhubuti ya kupambana na ugonjwa huo kwakuwa suala hilo si la hospitali peke yake.

Sababu za kurejea kwa ugonjwa huo kwa kasi, alisema Dk. Mzee, ni wananchi kukosa maji safi na salama na kuamua kutumia yayotoka kwenye makorongo.

Aidha, kutokana na mvua zilizonyesha, alisema, vyoo vya wakazi wengi vimebomoka na kupelekea kujisadia vichakani ambako kunachangia sana katika kueneza ugonjwa huo.

Habari Kubwa