Kipindupindu chaua watu 80

25Nov 2018
Beatrice Shayo
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Kipindupindu chaua watu 80

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amesema watu 4, 450 wameugua kipindupindu na 80 wamepoteza maisha tangu kuanza mwaka huu.

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, picha na mtandao

Hayo aliyasema jijini Dar es Salaam, wakati alipokuwa akizindua teknolojia mpya ya Lifestraw ambayo inachuja maji na kuzuia vijidudu vya kueneza magonjwa kwa asilimia 99.9.

Mwalimu alisema kinachosababisha kuendelea kuwapo kwa kipindupindu ni kukosekana kwa maji salama.

“Nimekuwa nikilaumiwa kuwa kipindupindu bado kipo lakini ukweli changamoto kubwa ni kukosa maji safi na salama,” alisema
Alisema alipoona kipindupindu hakiishi alimuomba Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa awaite mawaziri mbalimbali ili kujadiliana jinsi gani ya kutokomeza ugonjwa huo.

Aidha, alisema teknolojia hiyo mpya anaamini itasaidia kuondoa tatizo la kipindupindu pamoja na watu kupata maji yenye salama.

“Kuanzia Januari hadi leo Watanzania 4, 450 wameugua kipindupindu na tumewapoteza wengine 80, tunajua wamekula kinyesi na sababu kubwa ni maji yasiyo salama,” alisema

Alisema takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha kuwa asilimia 60 ya wagonjwa ambao wanahudhuria katika vituo vya afya wanaugua magonjwa ya kukosekana kwa usafi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Direct Solutions, Fatma Rashid, alisema maji safi na salama ya kunywa ni muhimu kwa binadamu na ndiyo maana wameamua kushirikiana na Vestergaard kuleta bidhaa za Lifestraw ili kuwaokoa wananchi na maradhi ya milipuko ikiwamo kipundupindu.

Rashid alisema Vestergaard inatumia mbinu ya kuchuja maji ambayo inazuia vijidudu vya magonjwa katika mazingira na inaweza kutumika hata katika vituo vya afya.

Habari Kubwa