Kirikuu NMB Bonge la Mpango zaenda Mbalizi na Mpanda

25Oct 2021
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Kirikuu NMB Bonge la Mpango zaenda Mbalizi na Mpanda

WASHINDI wawili wametangazwa baada ya kushinda pikipiki za miguu mitatu aina ya Sky Mark kwenye awamu ya pili ya kampeni ya Weka Akiba na Ushinde inayoendeshwa na Benki ya NMB 'NMB Bonge la Mpango - 2merudi Tena'.

Washindi hao ni Melkiadi Kepa wa Usongwe mkoani Mbeya na Anthony Meshack wa Mpanda mkoani Rukwa, NMB Bonge la Mpango ni kampeni itakayoendeshwa kwa wiki 12, ikilenga kuhamasisha utamaduni chanya wa kujiwekea akiba, ambako washindi 50 watajinyakulia pikipiki za mizigo 50 zenye thamani ya Sh. milioni 225, huku washindi 120 wakitarajia kujishindia fedha taslimu Sh. milioni 12.

 

Droo hiyo ilifanyika Ofisi za NMB Tawi la Magomeni mkoani Dar es Salaam, ambako Melkiadi wa NMB Tawi la Mbalizi Road na Anthony wa Tawi la Mpanda, ni kati ya washindi 12, ambako 10 miongoni mwao walishinda fedha taslimu Sh. 100,000 kila mmoja. Pikipiki mbili za Sky Mark ina thamani ya Sh. milioni 4.5.

 

Akizungumza kabla ya kuchezeshwa kwa droo hiyo, Meneja wa NMB, Tawi la Magomeni, Mary Marungi, alisema NMB Bonge la Mpango ni kampeni ya kimkakati, inayolenga kuhamasisha utamaduni chanya wa kutumia huduma za kibenki kwa kuweka ili kuwezesha utimilifu wa malengo ya mtu mmoja mmoja, kikundi ama taasisi.

 

"Kampeni hii ilizinduliwa Oktoba  mwanzoni na itadumu Desemba, ambako kila wiki tutakuwa tukiwazawadia washindi 12, kati yao 10 watashinda fedha taslimu na wawili wanajinyakulia pikipiki za miguu mitatu aina ya Sky Mark zenye thamani ya Sh. milioni 4.5 kila moja.

 

"Ili kushindania zawadi hizo, mteja mwenye akaunti anapaswa kuweka akiba isiyopungua Sh. 100,000 na yule ambaye hana akaunti, anatakiwa kufungua na kuweka akiba isiyokuwa chini ya kiasi hicho na moja kwa moja ataingia katika droo zetu hizi za kila wiki.

 

"Wito wetu kwao ni kuwataka waendelee kuweka akiba, ambapo licha ya kuwa njia ya kuwawezesha kufanikisha malengo yao, pia itawapa nafasi ya kujishindia zawadi hizi muhimu, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa mwaka na mwanzo wa mwaka ujao, ambako kunakuwa na sikukuu na pia malipo mbalimbali ya ada za watoto shuleni," alisema Marungi.

 

 

Droo hiyo ilichezeshwa mbele ya Pendo Albert Mfuru, ofisa kutoka Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), aliyesema jukumu lake katika tukio hilo ni kuhakikisha vigezo na masharti yanayosimamia michezo hiyo vinafuatwa, huku akiwahakikishia wateja wa NMB kuwa bahati nasibu hiyo inaendeshwa kihalali na washindi wake wanapatikana bila upendeleo wowote.

 

Washindi 10 walioibuka na zawadi ya fedha taslimu katika droo hiyo ni Keneth Mkumbo, Hadija Abbi, Rose Nungu, Nesha Mlaki, Selina Mwalugaja, Mwanahamisi Mwingira, Ado Mbunda, Dismas Simsonga, Emmanuel Kirenga na Shabani Kalinga.

0000000000

Habari Kubwa