Kisa baba kuchinja wanawe  mapacha, kukabidhi Biblia

17Apr 2018
Lilian Lugakingira
 BUKOBA  
Nipashe
Kisa baba kuchinja wanawe  mapacha, kukabidhi Biblia

RESPICIUS Diocress, mkazi wa kijiji cha Butayaibega wilayani Bukoba mkoani Kagera anatuhumiwa kuchinja kwa panga na kuwatenganisha kichwa na kiwiliwili watoto wake wawili mapacha.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi.

Aidha, imeelezwa baada ya kuwachinja mapacha hao wenye umri wa miaka minne Diocress alimkabidhi mwanawe mkubwa, Japhet Respicius (5) Biblia ili awaombee marehemu kisha yeye kutoroka na sasa wanakijiji wenzake wameazimia kumsaka.

Akizungumza kwa niaba ya wanakijiji hao, afisa mtendaji wa kijiji cha Butayaibega, Geofrey Deogratias alisema tukio hilo lilitokea saa saba usiku wa kuamkia Jumapili.

“Nilifika eneo la tukio na kukuta miili ya watoto Devotha Nyangoma Respicius (4) na pacha mwenzake Johanes Kato Respicius (4) ikiwa imelazwa sebuleni katika nyumba ya mtuhumiwa, huku vichwa vyao vikiwa pembeni mwa miili hiyo” alisema.

“Huyu mtuhumiwa alikuwa na watoto watatu ndani ya nyumba yake, lakini mtoto mmoja Japhet Respicius (5) hakumuua na alishuhudia baba yake akifanya unyama huo kwa wadogo zake.” 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwa polisi wanaendelea kumtafuta mtuhumiwa ili achukuliwe hatua za kisheria.

Mtendaji huyo alisema baada ya kuona hali halisi alipiga simu polisi kutoa taarifa juu ya tukio hilo, ambao walifika na kuichukua miili hiyo kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Alisema alipofika eneo la tukio alimkuta mtoto mkubwa akiwa nje ya nyumba akilia, na kuwaeleza kuwa baada ya baba yao kuwachinja wadogo zake alimkabidhi Biblia na kumsihi aendelee kuwaombea.

“Mtuhumiwa baada ya kutekeleza mauaji hayo alitoroka na kuelekea kusikojulikana, lakini ameendelea kutuma ujumbe mfupi wa maandishi kwa mwenyekiti wa kijiji, mtendaji na baadhi ya wanafamilia” alisema mtendaji Deogratias.

Alisema kuwa sehemu ya ujumbe huo ilisomeka: “Mwambie bibi Geogina ambaye ni bibi wa mke wangu aitwaye Kokwenda David kuwa nimekwishatekeleza alichokitaka kwa kuwaua Nyangoma na Kato, na mimi niko salama ila bado nawatafuta wengine wawili ili niwaue na kujipeleka polisi mwenyewe, msinitafute.”

Alisema baada ya polisi kuchukua miili ya marehemu hao, mtuhumiwa alirudi tena eneo la tukio akiwa na panga mkononi na kufyeka migomba yake na kuchoma nyumba yake moto, huku akiwatishia ndugu na jamaa zake kuwa wakimsogelea atawafyeka, na baadae alikimbia.

SHINDWA KULALA

Wakazi wa kijiji hicho, akiwamo Adiventina Sospeter ambaye ni shangazi wa mtuhumiwa na Gozberth Simon walisema walishindwa kulala usiku kucha kwa kuhofia kuvamiwa na mtuhumiwa huyo, maana hawafahamu wawili hao ambao bado Diocress anataka kuwaua ni akina nani.

Wananchi hao walitumia fursa hiyo kuliomba jeshi la polisi kufanya msako mkali kumkamata mtuhumiwa huyo kabla hajasababisha madhara makubwa zaidi kwa wananchi na ndugu zake wengine.

Naye mwenyekiti wa kitongoji cha Bulambizi lilipotokea tukio hilo, Dickson Balongo alisema kuwa kwa sasa wamedhibiti maeneo yote yanayoingia na kutoka kijijini hapo, ili waweze kumkamata maana wana imani amejificha katika kijiji hicho.

Taarifa kutoka eneo la tukio zilidai mtuhumiwa huyo aligombana na kutengana na mkewe Kokwenda ambaye ni mama wa watoto waliouawa, ambaye alichukuliwa na ndugu zake.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa juzi na muuguzi wa zamu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera iliyoko katika Manispaa ya Bukoba, Gloria Mpango, miili ya watoto hao ilionekana kutenganishwa vichwa na kiwiliwili wakati wa uchunguzi wa maiti hizo.

“Hapa uchunguzi umekwishafanyika, tunachosubiri ni polisi ili tujue ni hatua gani inafuata,” alisema Mpango.

 

Habari Kubwa