Kisutu yaibua kesi ya Lissu tuhuma uchochezi

02Jun 2020
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Kisutu yaibua kesi ya Lissu tuhuma uchochezi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam jana imetaja kesi inayomkabili aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, dhidi ya maneno ya uchochezi yenye lengo la kujenga chuki kwa wananchi kwa Rais John Magufuli.

Kesi hiyo iliyosajiliwa 279/2016, imetajwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mfawidhi, Godfrey Isaya.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, alidai kuwa kesi hiyo imepangwa kwa ajili ya kutajwa na upande wa Jamhuri umeomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Hata hivyo, alidai kuwa mshtakiwa alijidhamini mwenyewe katika kesi hiyo.

Lissu alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza katika kesi hiyo Agosti 6, 2016 na alisomewa mashtaka matatu ya uchochezi mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Cyprian Mkeha (kwa sasa Jaji wa Mahakama Kuu).

Kesi hiyo ni ya tatu kati ya kesi nne za uchochezi zinazomkabili katika mahakama hiyo.

Awali, upande wa Jamhuri ukiongozwa na Mawakili wa Serikali Wakuu, Faraja Nchimbi akisaidiwa na Paul Kadushi na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa, ulimsomea mashtaka yake mbele Hakimu Mkeha.

Kadushi alidai kuwa Agosti 2, 2016, katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Ilala, Dar es Salaam akiwa na nia ya kujenga chuki kwa wananchi dhidi ya Rais na serikali, alitoa maneno ya uchochezi na kunukuliwa: “Ukitaka kujua Magufuli ni dikteta uchwara ni pamoja na kauli zake.”

Alidai siku hiyo kwa nia ya kuleta dharau katika mfumo wa utoaji haki ndani ya mahakama na kuidharau alitoa maneno ya uchochezi kwa kwamba: “Kesi na mashtaka yenyewe ni ya kipuuzi na ya Kimagufuli gufuli.”

Vile vile, inadaiwa siku hiyo kulikuwa na mwenendo wa kesi mbili za jinai ambazo zilikuwa zimekwishamalizika na alitoa maneno akiwa na lengo la kudharau mienendo ya mahakama.

Alinukuliwa: "Siwezi kufungwa, kesi na mashtaka yenyewe ni ya kipuuzi na ni ya Kimagufuli”.

Upande wa Jamhuri ulipinga dhamana kwa madai kuwa ataingilia upelelezi.

Hata hivyo, jopo la mawakili tisa likiongozwa na Peter Kibatala, lilipinga hoja za Jamhuri kuzuia dhamana ya mshtakiwa kwamba anafahamika kuwa ni mbunge na dhamana ni haki yake.

Hakimu Mkeha alimtaka mshtakiwa kujidhamini mwenyewe.

Jana, Hakimu Isaya alipanga kesi hiyo kutajwa tena Julai mosi, mwaka huu.

Habari Kubwa