Kitambulisho cha taifa lazima kila Mtanzania

07Dec 2018
Na Mwandishi Wetu
Bunda
Nipashe
Kitambulisho cha taifa lazima kila Mtanzania

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amesema kupata kitambulisho cha taifa kwa kila Mtanzania ni jambo la lazima na kwamba mtu ambaye hatakuwa nacho atapa tabu sana.

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, picha na mtandao

Akizungumza na wananchi wa Kata ya Nansimo, Mwibara, Wilaya ya Bunda, mkoani Mara, Lugola, alisema uandikishaji ulishakamilika kwenye baadhi ya mikoa na ambao hawakuandikishwa kipindi kile na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), wanapaswa kwenda katika ofisi za wilaya za mamlaka hiyo ili waweze kujiandikisha.

“Wapo ambao kipindi kile NIDA wanaandikisha wananchi mitaani hawakuwapo hilo nalijua, na pia kuna wale ambao kipindi cha kuandikishwa kinafanyika walikua hawajafikisha miaka 18, hao wote ambao hawajaandikishwa wanapaswa sasa kwenda kujiandikisha haraka iwezekanavyo katika ofisi za NIDA katika wilaya zao,” alisema Lugola.

“Ndugu wananchi wa Mwibara na kote nchini, kupata kitambulisho ni jambo kubwa la nchi hivyo tusililinganishe na jambo lingine lolote na tusilichukulie kirahisi rahisi tu na nawaambia baada ya mchakato huu kuisha tukamkuta mtu hana kitambulisho maelezo yake yatakuwa ni magumu kueleweka kama kweli yeye ni Mtanzania halali na atapata tabu sana,” alisema Lugola.

Lugola ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mwibara, alisema suala la kupata kitambulisho cha taifa ni la lazima kwa kila Mtanzania aliye hapa nchini na ni kosa kubwa kama ni raia akaamua kukaidi ikiwa Rais Dk. John Magufuli ameamua kutoa vitambulisho hivyo bure bila malipo yoyote nchini.

Aidha, alisema Mkoa wa Mara umeshakamilisha kazi hiyo na kinachofanyika sasa ni kuhakiki, kuyafanyia kazi mapingamizi pamoja na uchakataji na itakapokamilika waliojiandikisha na ambao wana sifa watapewa vitambulisho vyao.

“Hakuna Mtanzania mwenye sifa atakayekosa kitambulisho cha taifa, lakini lazima muwe na subira wakati kazi ya utambuzi wa watu gani wanaweza kupata vitambulisho hivi, pia katika utambuzi tunapaswa kuwa makini sana kwa sababu tusije tukapenyeza wasio raia wasiostahili na wao wakaweza kupata vitambulisho na baadaye tukaja kupata shida,” alisema Lugola.

Habari Kubwa