Kitila asitisha taasisi kutoa huduma ya maji

17Oct 2018
Na Mwandishi Wetu
HAI
Nipashe
Kitila asitisha taasisi kutoa huduma ya maji

KATIBU Mkuu Wizara ya Maji, Prof. Kitila Mkumbo, amesitisha shughuli zote za Taasisi ya Maji ya WSTF iliyokuwa ikitoa huduma katika Mkoa wa Kilimanjaro na kuagiza kufanyika tathmini na uchunguzi wa kina wa mali za taasisi hiyo kabla ya kukabidhiwa serikalini.

KATIBU Mkuu Wizara ya Maji, Prof. Kitila Mkumbo.

Prof. Kitila alifikia uamuzi huo jana, baada ya Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, kumweleza kuwa taasisi hiyo imekuwa ikisababisha kuibuka kwa mgogoro kati ya serikali na bodi saba za watumia maji katika wilaya tatu.

Alisema katika hatua za muda mrefu za kunusuru shughuli za utoaji wa maji katika wilaya za Hai, Siha na Moshi Vijijini, zisiingiliwe na changamoto hiyo na serikali imeagiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi Mjini (Muwasa), kusimamia utekelezaji wa majukumu ya WSFT na kuhakikisha kuwa Bodi za Watumia Maji katika wilaya hizo zinaendelea kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

Pamoja na hatua hiyo, Prof. Kitila alisema serikali imeanza mchakato wa kuanzisha mamlaka ya maji katika maeneo husika ambayo ndiyo itakuwa na jukumu la kutoa huduma hiyo.

"Katika kuhakikisha kuwa changamoto zoinazoikabili WSFT haziathiri utoaji wa huduma ya maji kwa wananchi na kuweka mfumo endelevu katika wilaya hizo tatu, Wizara ya Maji imechukua hatua kusitisha shughuli za taasisi hii,’ alisema.

"Naomba nieleweke hapa kwamba, sisi kama wizara hatuna uhalali wala uwezo wa kufuta taasisi kisheria, uwezo wetu pekee ni kusitisha kutoa huduma zao katika sekta ya maji."

Alisema uamuzi huo unatoa fursa ya uchunguzi na kushughulikia changamoto za kisheria ili kukidhi matakwa ya sheria ya huduma za maji na usafi wa mazingira namba 12 ya mwaka 2009.

Aidha, wizara hiyo imeagiza kufanyika kwa tathmini ya mali zinazoendeshwa na WSFT wakati na baada ya kukabidhiwa mradi.

Taasisi hiyo ya WSFT ilikuwa imejipa jukumu la kufanya manunuzi ya vifaa vya miundombinu ya maji kama dira za maji, kufanya tathmini ya utendaji wa COWSOs (Bodi za Maji) na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa bodi hizo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, alisema taasisi hiyo licha ya kutoa huduma za maji ilikuwa haijawahi kusajiliwa kufanya kazi hizo jambo ambalo limesababisha kuwapo kwa mgogoro mkubwa kati ya serikali na bodi hizo.

Alisema serikali ya awamu ya tano imeelekeza nguvu kubwa katika kuhakikisha mwananchi wa kawaida ananufaika na rasilimali za nchi hali ambayo itawezesha kuondoa kero za maji kwa kutumia vyema rasilimali hizo.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Moshi (Muwsa), Prof. Faustine Bee, alisema ameyapokea maagizo ya serikali ya kusimamia huduma za maji katika maeneo yanayohudumiwa na WSFT kwa wilaya ya Hai, Siha na Moshi vijijini.

Habari Kubwa