Kitimtimu cha usafiri wa mabasi mikoani

20Dec 2017
Mary Geofrey
Nipashe
Kitimtimu cha usafiri wa mabasi mikoani

ZIKIWA zimebaki siku tano kabla ya kusherehekea sikukuu ya Krismas na baadaye Mwaka Mpya, abiri wanaosafiri kwenda mikoa mbalimbali nchini kutoka jijini Dar es Salaam, wanakumbana na adha mbalimbali za usafiri.

Abiria wakiwa wamekaa katika standi kuu ya Mabasi Ubungo baada ya gari walilokata tiketi la kampuni ya Ota linalofanya safari zake Dar es Salaam na Bukoba kutotokea tangu asubuhi kituoni hapo. PICHA: HALIMA KAMBI

Katika kituo cha mabasi Ubungo, jana Nipashe ilishuhudia abiria takriban 60 wakiwa wamekosa usafiri wa basi kutokana na kile kilichoelezwa kuwa lilikuwa likifanyiwa matengenezo.

Basi hilo aina ya Ota linalofanya safari kati ya Dar es Salaam na Bukoba mkoani mkoani Kagera, lilishindwa kutokea katika kituo hicho kikuu cha mabasi Ubungo tangu saa 11;00 alfajiri kuchukua abiria waliokuwa wameshakata tiketi kwa ajili ya kuanza safari.

Raphael Sospeter, mkazi wa Dar es Salaam, ambaye alitakiwa kusafiri jana na familia yake kwa kutumia basi hilo, alilalamikia hatua hiyo akisema walichofanyiwa ni ukiukwaji wa sheria na haki za abiria.

Alisema alilazimika kukata tiketi tangu Desemba 5, mwaka huu, kwa ajili ya kuepuka usumbufu unaotokana na ongezeko la abiria msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka.

“Tulifika asubuhi saa 11:00 alfajiri na hatukukuta gari na tulipouliza tukaambiwa bado halijafika. Ilipofika saa 12 asubuhi tukaenda kuuliza kwa askari walioko katika kituo hiki na wakasema wanaulizia na baadaye wakatujibu kuwa basi hilo halipo,” alisema.

Sospeter alisema askari walimjibu kuwa wamewasiliana na mmiliki wa basi, lakini hakupatikana na walipochunguza, walibaini kuwa gari walilotakiwa kupanda lilikuwa njiani likitokea mkoani Morogoro.

Msafiri mwingine, Vestina Kazungu, aliieleza Nipashe kuwa mbali na kukosa usafiri ilhali ni haki yao ya msingi, wamekumbana na changamoto ya kujibiwa kauli mbaya na makarani wa basi hilo.

“Kama unavyoona hapa tupo na watoto wadogo mpaka muda huu (saa 6:00 mchana) hatuoni dalili ya usafiri na hawa mawakala wa basi badala ya kutupa moyo, wanatujibu vibaya eti kwani ni mara yetu ya kwanza kusafiri hadi tuogope kuchelewa kuondoka kituoni,” alisema.

Naye Katibu Mkuu Msaidizi wa Chama cha Kutetea Abiria (Chakua), Maulid Masalu, alisema walichofanya ni kuhakikisha wanashughulikia usafiri wa abiria hao ili wasafiri. 

“Baada ya kupata malalamiko ya abiria, tulianza kushughulikia kwanza kufahamu lilipo basi hilo na kubaini kuwa wafanyakazi walidanganya kuwa lilikuwa likitengenezwa kumbe lilikuwa njiani kuja jijini Dar es Salaam,” alisema Masalu.

Alisema basi hilo lilitakiwa kuwa limefika jijini Dar es Salaam juzi usiku, lakini ilishindikana kutokana na kupata hitilafu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Jumanne Muliro, aliieleza Nipashe jana kuwa  abiria 54 walikwama katika kituo hicho cha mabasi.

Alisema wanawashikilia mawakala wanne wa kampuni hiyo kwa tuhuma za kujipatia fedha kwa udanganyifu na kwamba wanaendelea na upelelezi. Alisema uchunguzi utakapokamilika watafikishwa mahakamani.

“Watu hawa tunawashikilia na tunashirikiana na mawakili wa serikali ili tuweze kuwafikisha mahakamani. Pia tunamsaka mmiliki wa basi ambaye naye tutamchukulia hatua za kisheria,” alisema Kamanda Muliro.

Alisema mmiliki na watumishi wa basi hilo, ameshindwa kutimiza makubaliano waliyoweka na abiria kwa kushindwa kuwasafirisha hadi jana mchana.

Kadhalika alisema, basi hilo liliwasili katika kituo hicho saa 7:00 mchana na lilifanyiwa uchunguzi ili kufahamu kama linaweza kuendelea na safari au la.

“Tukibaini halina tatizo abiria walio tayari watasafiri na basi na watalala Dodoma na ambao hawako tayari  kuondoka tena watarejeshewa nauli zao kwa sababu ni haki yao kisheria,” alisema.

Pia alisema endapo abiria hao watashindwa kuondoka, mmiliki wa basi atatakiwa kuwalipia gharama za chakula na malazi.

Abiria waonywaKamanda Mliro pia aliwataka abiria kuwa makini katika msimu huu wa kuelekea sikukuu kwa kuhakikisha wanakata tiketi za mabasi kwenye ofisi husika.

“Abiria asikate tiketi barabarani hata kama mtu amevaa sare. Usikate tiketi kwake ili kuepuka matapeli, usumbufu au kulipa fedha nyingi zaidi. Hakikisha unakata katika ofisi za basi husika,” alisema.

Aidha, alisisitiza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kuimarisha ulinzi na kuongeza kasi ya ukaguzi wa mabasi katika kituo hicho na kwamba mabasi yenye hitilafu hayataruhusiwa kusafiri.

Habari Kubwa