Kitimtimu NCCR Mbatia kusimamishwa uenyekiti

22May 2022
Beatrice Shayo
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Kitimtimu NCCR Mbatia kusimamishwa uenyekiti

​​​​​​​KITIMTIMU kimeibuka ndani ya NCCR Mageuzi baada ya Halmashauri Kuu ya chama hicho kutangaza kumsimamisha Mwenyekiti wake, James Mbatia, kutojihusisha na shughuli zozote pamoja na Makamu Mwenyekiti Bara, Angelina Mtahiwa, hadi mkutano mkuu utakapoitishwa ili wajieleze kuhusiana na-

James Mbatia.

-tuhuma zinazowakabili.

Wakati hayo yakitokea, uongozi wa chama hicho kupitia kwa msemaji wake, umesema kilichofanywa ni uhuni na kwamba Mbatia bado ni mwenyekiti halali wa chama hicho.

Uamuzi huo ulifanyika jana kutokana na tuhuma mbalimbali zinazodaiwa kuwakabili viongozi hao, ikiwamo kugombanisha viongozi na kulazimisha kujiuzulu.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya NCCR-Mageuzi na Mwenyekiti wa azimio hilo, Joseph Selasini, ndiye aliyetangaza maazimio hayo ya kusimamishwa kwa viongozi hao, na kueleza kuwa pia wamelivunja Baraza la Wadhamini la NCCR na kuteua wajumbe wapya ambao watasajiliwa kwa mujibu wa taratibu zitakazowekwa.

Akisoma maazimio ya halmashauri kuu, Selasini alitangaza kumsimamisha Mbatia katika wadhifa huo kwa kile alichoeleza ni kutokuwa na uhusiano mzuri na makatibu wake.

Selasini alisema sababu nyingine ni Mbatia anatuhumiwa kwa kukisababishia chama hicho kisishiriki mikutano mbalimbali iliyoitishwa kwa ajili ya kujadili masuala ya demokrasia ya vyama vingi, ikiwamo ule ulioitishwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).

Alisema alisema maazimio ya kumsimamisha Mbatia ni halali kwa kuwa akidi ya wajumbe wake ilikidhi matakwa ya kisheria waliohudhuria walikuwa 52 kati ya wajumbe 82.

MBATIA AFUNGUKA

Baada ya kutangazwa kwa taarifa hiyo, Mbatia alisema hatambui mkutano uliofanyika wa halmashauri kuu wa kumsimamisha na kusisitiza kwamba kikao hicho ni batili.

Alisema hakuna kikao kilichofanyika na kwamba atamshangaa Msajili wa Vyama vya Siasa endapo atabariki maazimio ya mkutano huo, akisema anajadiliana na wanachama wenzake kuona hatua za kuchukua.

Mbatia alisema juzi waliwasilisha taarifa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kuhusu kikao cha kamati kuu kusogeza mbele mkutano na kumweleza wamemsimamisha kazi Katibu Mkuu wa chama hicho, Matha Chiumba.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha NCCR- Mageuzi, Edward Simbeye, alisema kikao kilichofanyika cha kumsimamisha Mbatia siyo cha kihalali na kwamba watakwenda kupambana na Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kuwa ndiye adui wao namba moja katika mgogoro huo.

Simbeye alisema vyama vyote vinaendeshwa kwa mujibu wa katiba na kwamba wajumbe hao hawakuwa na mamlaka ya kumsimamisha Mbatia na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho.

Simbeye alisema watu hao pia hawana mamlaka ya kikatiba, ndiyo maana hawaonekani ofisini, huku akiwaita ni wahuni.

“Watanzania na wanachama wa NCCR-Mageuzi popote walipo nchini leo hatukuwa na kikao cha Halmashauri Kuu kilichofanyika Kurasini ambacho kimeongozwa na Joseph Selasini

“Ni uhaini ndani ya chama na uhuni ambao sisi wanachama vijana, wazee wapenda demokrasia katika taifa letu hatuwezi kukubali uhuni uliofanyika,”alisema Simbeye

Alisema kutokana na kilichotokea hawawezi kuuvumilia na kwamba chama kitakaa katika utaratibu ambao unafaa wa vikao na kufanya maamuzi.

Alisema chama cha NCCR-Mageuzi ni chama cha Watanzania, kimesajiliwa kwa mujibu wa katiba na yoyote ambaye wataona anavunja katiba ya nchi hawako radhi kumuona akiendelea kubaki kwenye ofisi ya umma.

Simbeye alisema aliyeitwa Katibu Mkuu wa chama alisimamishwa kujibu tuhuma zinazomkabili Mei 15, mwaka huu katika kikao cha kamati kuu.

“Kikao cha Halmashauri Kuu kinaendeshwa na Selasini na kuvunja bodi ya wadhamini Are they serious? Unaweza kuvunja bodi ya wadhamini kihuni huni na kumsimamisha mwenyekiti wa chama huo uhuni hatuwezi kuukubali chama chetu kipo imara,”alisema Simbeye.

Alisema NCCR-Mageuzi kina uzoefu wa kupambana na migogoro ya aina hiyo, hakuna ambaye ataweza kukiua chama hicho, kwamba atakayedhubutu kufanya hivyo Mwenyezi Mungu anaweza kumchukua yeye kabla ya kukichukua chama hicho.

KAULI YA MSAJILI

Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Sisty Nyahoza, alisema ofisi yake ni mlezi wa vyama vya siasa vyenye usajili kamili na wanavilea kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa.

Alisema hata wiki iliyopita alikuwa kwenye mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ofisi ya msajili ilialikwa kwa sababu walikuwa na mchakato wa kuwateua wajumbe wa bodi ya wadhamini.

Kisheria, alisema  chama kinavyofanya mabadiliko katika bodi ya wadhamini lazima kuwapo na ofisa wa serikali kwa ajili ya kutazama mchakato huo, kwamba wadhamini wanateuliwa kwa mujibu wa katiba.

Nyahoza alisema kwa upande wao wameshuhudia yaliyotokea wanasubiri taarifa rasmi waipokee kutoka NCCR-Mageuzi ndipo watatoa msimamo.

Alisema kikao wameona kimefanyika na wajumbe walikuwapo sambamba na viongozi.

“Nimeona kilichofanyika wajumbe walikuwapo akidi imesomwa na ninyi mmeshuhudia wakijitambulisha na sisi tuna orodha yetu ya wajumbe ofisini tutaenda kulinganisha na ile ya ofisini. Lakini wajumbe wamesomwa na akidi imesomwa vizuri kwa maana ya kutimia. Ni kikao halali na utaratibu unaonekana umefuatwa kwa mujibu wa katiba yao kwa kuwasimamisha,” alisema.

Alisema utaratibu umefuatwa vizuri na mambo mengine watayatizama kwa namna taarifa watakavyopatiwa ofisini na kuangalia kwa mujibu wa katiba na kanuni na kujipa muda kwa ajili ya kuipitia na kutoa msimamo.

Habari Kubwa