Kivuko cha Mv. Ukara II kuwafuta machozi wananchi Mwanza

19Oct 2020
Neema Emmanuel
MWANZA
Nipashe
Kivuko cha Mv. Ukara II kuwafuta machozi wananchi Mwanza

Maelfu ya wakazi wa Ukara na Bugolola wilayani Ukerewe mkoani Mwanza wamejitokeza kuipokea kivuko kipya cha Mv.Ukara II (Hapa Kazi Tu) ambayo ni mbadala wa MV.Nyerere iliyozama September 20 mwaka  2018, na kupelekea watu takribani 227 kupoteza maisha.

Akizungumza wakati akizindua kivuko hicho leo Oktoba 19,2020, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe ameagiza Shirika la Uwakala wa Meli Nchini (TASAC) kuhakikisha inaweka maofisa usimamizi katika maeneo yote ya usafiri majini sambamba na kutoa mafunzo kwa wa wamiliki na waendeshaji wa vyombo vya majini ikiwamo Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA).

Amesema kuwa hatua hiyo itasaidia  kuongeza ufahamu juu ya umuhimu wa kuzingatia utaratibu na kanuni zinazosimamia uendeshaji  wa vyombo hivyo kuepuka matukio ya ajali.

Aidha, ameagiza TEMESA kusimamia kwa ukaribu uendeshaji wa vivuko hivyo ili wananchi wafaidi matunda ya Serikali maendeleo yao binafsi.

Kamwelwe amesema kuwa kivuko hicho kina ubora kwa kuwa kimewekewa mfumo maalum ambao unaweza kutambua uzito wa mzigo, abiria pamoja na tarehe ya kufanyiwa matengenezo, huku akitangaza wananchi wa eneo hilo kusafiri bure katika Kivuko jicho kwa siku mbili kuanzia leo.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya ujenzi) Elias Mwakalinga amesema Serikali imekamilisha ujenzi wa vivuko saba zikiwemo  Ambulance maalum tatu kwa ajili ya kusaidia usafiri katika mikoa mbalimbali vyenye thamani ya Sh. Bilioni 36.3.

"Kwa miaka mitano serikalli imejenga vivuko saba pamoja na Ambulance maalum tatu pia kwa sasa timu ya watalaam ipo mkoani Mwanza kwa ajili ya kufanya utafiti ili kubaini maeneo yanayohitaji vivuko na kuyaanisha," amesema Mwakalinga na kuongeza kuwa;

"Baada ya ajali ya Mv.Nyerere, Serikali kupitia Wizara iliamua kununua kivuko mbadala chenye urefu wa mita 42 na upana wa mita 10 na chumba maalumu cha kujifungulia wanawake wajawazito hiyo ni kwa sababu serikali inawajali akina mama," amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella amesema wana mshukuru Rais Magufuli kwa kazi kubwa aliyoifanya kwani kivuko hicho kimetengenezwa ndani ya miaka miwili.

"Tunamshukuru sana Rais John Magufuli kwa kazi kubwa aliyoifanya, ndani ya miaka miwili kutuletea kivuko, nchi yetu imshukuru Mungu sana kwa kupata kiongozi mahili mwenye maamuzi na anayeguswa na shida za wananachi na kwamba ukamilishwaji wa kivuko hicho ni fursa kubwa ya kiuchumi," amesema Mongella na kuongeza kuwa;

"Kupitia kivuko hiki biashara zitazidi kuboreka na vipato vya wananachi vitazidi kuimarika, usafiri ni sekta nyeti kwa maendeleo ya wananchi hivyo amewataka kuitumia meli hiyo kuzalisha ili kupandisha uchumi wao ." ameeleza Mongella.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya hiyo, Cornel Magembe amesema tangu ilipotokea ajali ya Mv.Nyerere mwaka 2018, wananchi walikabiliwa na shida ya usafiri hiyo wanaishukuru Serikali kwa kusema na kutenda na kuwaletea kivuko.

"Kwa niaba ya wananchi natoa shukrani kwa Rais  Magufuli baada ya kutekeleza ahadi yake aliyoitoa baada ya kuielekeza Wizara ya Ujenzi kuunda kivuko kipya ambacho itatatua changamoto ya usafiri katika eneo hili kwani watu walipata tabu sana sasa wamepata kivuko cha kutumia dakika 40 kutoka Bwisya kwenda Bugolola ambapo awali walitumia masaa mawili" amesema Magembe.  

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adamu Malima,  amesema kuzinduliwa kwa kivuko hicho ni nuru kwa wakazi wa maeneo hayo, Watanzania ni wamoja hivyo wananchi wasikubali maneno ya kutenganishwa yanayotolewa na baadhi ya watu bali waimariashe mshikamao.

Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Japhet Masele amesema, gharama za ujenzi wa kivuko hicho ni Billion 42.2 ambazo zimetolewa na Serikali chenye uwezo wa kubeba abiria 300 ,magari 19 na mizigo tani 100.

Amesema kivuko hicho kimetengenezwa  na kampuni ya Songoro Marine iliyopo Jijini Mwanza, kivuko hicho kitawaondolea adha wakazi wa eneo hilo pia ni jukumu la serikali kuwapeleka huduma wananchi pale panapohitajika pia aliwataka wakitunze kivuko hicho.

Habari Kubwa