Kiwanda kikubwa cha mbolea kujengwa nchini

22Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Kiwanda kikubwa cha mbolea kujengwa nchini

KANSELA wa Ujerumani, Angela Merkel, juzi amezungumza kwa njia ya simu na Rais Dk. John Magufuli na kumhakikishia kuwa Ujerumani ipo tayari kukuza zaidi uhusiano wake na Tanzania hususani kusaidia juhudi za kuimarisha uchumi.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, ilisema Markel amempongeza Rais Magufuli kwa juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kujenga mazingira mazuri ya uwekezaji ikiwamo kupambana na rushwa na kuimarisha miundombinu.

Kufuatia mafanikio hayo Markel amesema Ujerumani itawaleta wafanyabiashara watakaowekeza katika maeneo mbalimbali ya kuimarisha uchumi ikiwamo kujenga kiwanda cha kuzalisha mbolea, ambacho kitakuwa kikubwa kuliko vyote barani Afrika.

Merkel alisema Ujerumani imedhamiria kuunga mkono juhudi za ujenzi wa viwanda nchini Tanzania na kwamba ana matumaini kuwa kiwanda kikubwa cha mbolea kitakachojengwa nchini kitasaidia kuongeza kipato cha wananchi na kuimarisha kilimo na nchi nyingine za Afrika.

Alitoa wito wa kuimarishwa kwa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) na kumwalika kwa mara ya pili Rais Magufuli kutembelea Ujerumani, ziara ambayo itatanguliwa na ziara ya mawaziri wa Tanzania kukutana na mawaziri wa Ujerumani.

Kwa upande wake Rais Magufuli alimshukuru Merkel kwa kumpigia simu na kueleza dhamira yake ya kukuza zaidi uhusiano wa Tanzania na Ujerumani na kubainisha kuwa Tanzania itahakikisha inajenga mazingira mazuri katika maeneo yote ya ushirikiano yakiwamo ya biashara na uwekezaji.

Rais Magufuli alimpongeza Markel kwa uongozi wake wa zaidi ya miaka 13 akiwa Kansela wa Ujerumani na amemhakikishia kuwa Tanzania itadumisha na kukuza zaidi ushirikiano huo kwa manufaa ya pande zote mbili.

Habari Kubwa