Kiwanda kilichozinduliwa na Samia chasimamisha uzalishaji

17Oct 2021
Na Mwandishi Wetu
Tarime
Nipashe Jumapili
Kiwanda kilichozinduliwa na Samia chasimamisha uzalishaji

Hali ni tete katika kiwanda cha chaki cha Victoria kinachomilikiwa na kampuni ya Arwa Investment kilichopo wilayani Tarime, baada ya kukosa soko la kuuza chaki mkoani Mara.

Kiwanda hicho kilichozinduliwa na Rais Samia Suluhu wilayani Tarime wakati huo akiwa ni Makamu wa Rais.Imeelezwa kuwa licha ya mkoa wa Mara kuwa na shule nyingi za msingi na Sekondari na vyuo lakini hazinunui chaki zinazozalishwa na kiwanda hicho badala yake zinazonunuliwa ni za kutoka mikoa mingine na nchi jirani ya Kenya zinazouzwa  kwenye  steshenari mbalimbali.

Meneja uzalishaji kiwanda cha Victoria Magala Magembe alisema kuwa kitendo cha bidhaa za ndani kutonunuliwa kunarudisha nyuma jitihada za wawekezaji wa ndani kwa kuwa watu wengi hawapendi kununua bidhaa za kwao na kukimbilia bidhaa za nje.

"Kiwanda kilianza uzalishaji 2017 kilizinduliwa na Rais Samia wakati huo akiwa Makamu wa Rais tuna miezi sita sasa kiwanda kimesimama uzalishaji  kwasababu chaki hazinunuliwi,box moja la chaki lenye paketi 30 na kila paketi ikiwa na chaki 100 ni sh.37,500.

"Awali  tuliuza box1,500 kwa mwezi,tukasema labda kwakuwa kiwanda ni kipya lakini mauzo yameendelea kupungua,mwezi uliopita tumeuza box 12 kikifa ni hasara kubwa kwa kiwanda,kiwanda kipo Tarime lakini chaki zinazonunuliwa ni za nje ya Mara na nchi jirani ya Kenya nawakati chaki zetu zimezingatia ubora na vigezo vyote vya TBS" alisema Magala.

Meneja wa kiwanda hicho Nyanjo Migire alisema kuwa tatizo la ununuzi wa chaki siyo rafiki ikizingatiwa shule ndiyo wanunuzi wakuu wa chaki lakini hawanunui kiwandani zaidi ya kununua madukani nakwamba aliyewahi kuwa mkuu wa mkoa Mara Charles Mlingwa alipambana kuhakikisha bidhaa za viwanda vya ndani zinanunuliwa.

"Tulishaomba halmashauri zetu zitusaidie kuhamasisha chaki za kiwandani zinunuliwe lakini ikashindikana,kule Simiyu shule zote zinanunua chaki za kiwanda chao lakini huku Mara huo utaratibu haupo mkoa wenyewe bado haujathamini kiwanda chao hii itawakatisha tamaa watu waliokuwa na nia ya kuwekeza Mara kwakuwa bidhaa za ndani hazithaminiwi".

" Soko likikosa kiwanda kitakufa halmashauri itakosa ushuru wa huduma 0.3,kodi TRA,TBS,NEMC,BAKODI,kodi ya Umeme na maji,Malighafi tulizokuwa tunanunua Singida hazitanunuliwa na ajira hazitokuwepo na mwenye kiwanda atapata hasara" alisema Migire.

Mwita Marwa mkazi wa mtaa wa Bomani alisema kuwa baadhi ya walimu wanamiliki steshenari pesa zinapoingia kwenye akaunti ya shule uzichukua nakununua chaki kwenye halmashauri zao hivyo hawezi kwenda kununua kiwandani wakati wana maduka yanayouza chaki.

Lucy James mkazi wa mtaa wa Rebu alisema kuwa"shida unakuta kwenye manunuzi kuna makubaliano kwamba ntakuwa nanunua chaki kwako lakini na Mimi unanikatia changu 10,000 au 15,000 sasa pale kiwandani hakuna"

"Wewe jiulize chaki za kiwanda cha Victoria box moja linauzwa 37,500 lakini utakuta wananunua chaki za nje ya Tarime zinazouzwa kwenye steshenari kama chaki za Continental,Dobercolor na zinginezo zinazouzwa box moja sh. 45,000 -50,000 hapo ndo ujue kuna jambo la siri lenye manufaa kwa wakuu wa shule na idara ya elimu" alisema Lucy.

Mwenyekiti wa halmashauri ya mji Tarime  ambaye pia ni diwani kata ya Nkende Daniel Komote amewataka wamiliki wa viwanda vya ndani na wajasiliamali kuzitangaza bidhaa zao nakwamba baadhi ya bidhaa hazinunuliwi kwasababu watu hawafahamu zinakopatikana.

"Hicho ni kiwanda chetu cha ndani ni vyema wenye kiwanda wakafika halmashauri kutangaza bidhaa zao ili tuwasaidie kuwatangazia,tuna vikao vyetu vya baraza la madiwani aje tumpe hata dakika kumi atangaze bidhaa yake ili hata madiwani wakienda huko kwenye kata zao wanamtangazia.

" watualike madiwani tutembelee kiwanda chake tujue changamoto ili zitatuliwe wanapokaa kimya hatuwezi kufahamu kinachoendelea kwenye kiwanda"alisema Komote.

Komote alisema kuwa uwekezaji wa viwanda unachangia maendeleo kwakuwa wananchi upata ajira na halmashauri upata ushuru wa huduma hivyo wamiliki wa viwanda na wajasiliamali wanajukumu la kuzitangaza bidhaa zao itasaidia kupata masoko. 

Habari Kubwa