Kiwango duni cha elimu chatajwa kuwa tatizo kuukabili mfumo dume

26Jul 2021
Pendo Thomas
KIGOMA
Nipashe
Kiwango duni cha elimu chatajwa kuwa tatizo kuukabili mfumo dume

Wanawake wasio na kiwango kikubwa cha elimu wametajwa kushindwa kuukabili mfumo dume kwenye jamii katika kufanya maamuzi ya idadi ya watoto wa kuzaa hivyo kujikuta wakizaa watoto karibu karibu hali ambayo imekuwa kisababishi cha vifo vitokanavyo na uzazi.

Mganga Mkuu Wilaya ya Kasulu, Robert Rwebangira amesema licha ya wanawake kupata elimu ya afya ya uzazi na namna ya kupishanisha watoto itolewayo na wahudumu wa afya lakini imekuwa ngumu kufikia malengo kutokana na utamaduni kandamizi ambao umekuwa ukiwasababisha mwanamke kushindwa kujisimamia hivyo kurudisha nyuma jitihada za serikali katika kudhibiti vifo vitokanavyo na uzazi.

Amesema katika utendaji kazi wake amebaini asilimia kubwa ya wanawake wanaoshindwa kujisimamia katika masuala ya uzazi ni wale walioishia darasa la saba na ambao hawajenda shule kabisa hivyo kuziomba familia kuhimiza mtoto wa kike kupelekwa shule .

"Tukubali suala la uamuzi wa idadi ya watoto wa kuzaa na kupishanisha limegubikwa na mfumo dume"Alisema Rwebangira.

Rwebangira amesema kitaalamu inapaswa mtoto azaliwe wakati aliyemtangulia akiwa umri wa miaka mitatu ili kutoa nafasi kwa afya ya mama na mtoto ikiwemo mtoto kunyonya kwa miaka miwili.

Alieleza mwanamke kushindwa kupishanisha watoto inasababisha watoto kuzaliwa wakiwa na kilo pungufu chini ya kilo 2.5 au chini ya hapo hali ambayo pia husababisha watoto wengi wa aina hiyo kupoteza maisha kutokana na kuhitaji uangalizi mkubwa ili kilo zao ziongezeke.