KKKT yaja na hatua za ziada

30Mar 2020
Godfrey Mushi
Hai
Nipashe
KKKT yaja na hatua za ziada

KANISA la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), limesema wakati wowote kuanzia sasa, litachukua hatua za ziada katika kukabiliana na kasi ya maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona.

Mkuu wa KANISA la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Frederick Shoo. picha mtandao

Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa kanisa hilo, Askofu Dk. Frederick Shoo, jana wakati akihubiri katika ibada maalum ya kumsimika Mchungaji Biniel Mallyo, kuwa Mkuu wa Jimbo la Hai la Dayosisi ya Kaskazini ya KKKT.

Mchungaji Mallyo anabeba mikoba hiyo, baada ya mtangulizi wake, Mch. Aminirabi Swai, kufariki dunia Julai mwaka jana.

"Ndugu zangu katika kukabiliana na janga hili la ugonjwa wa corona, huenda tukachukua hatua za ziada katika taratibu zetu za ibada, ingawa hatutaacha kumwabudu Mungu.

"Pamoja na tahadhari zote, hatutaacha kumlilia Bwana ili atuepushe na janga hili na kutuponya. Amesema niite nami nitaitika. Tutamlilia nani zaidi ya Mungu ambaye ni kimbilio letu."

Akihubiri katika Usharika wa Hai Mjini, Askofu Dk. Shoo ambaye ni Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini, alisema huu ni wakati wa kumkaribia Mungu, kwa kuwa inaonekana kwa nguvu zetu na akili zetu za kibinadamu, hatuwezi zaidi ya kimkimbilia yeye.

Aliwatia matumaini Watanzania, akieleza kuwa ugonjwa huo wa corona utapita maana Mungu amesema atawalinda dhidi ya mauti na magonjwa.

Pamoja na mambo mengine, Askofu Dk. Shoo aliwasihi Wakristo nchini kuwaombea watumishi wa sekta ya afya wanaotoa huduma dhidi ya waliothibitika kuugua ugonjwa huo.

Alitangaza maombi maalum nchi nzima, akitaka kuomba Mungu aliepushe taifa na ongezeko la wagonjwa wa corona.

Kabla ya kuanza kwa ibada hiyo, timu ya madaktari na maofisa wa idara ya afya Wilaya ya Hai, ikiongozwa na Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk. Irene Haule, iliwapima waumini zaidi ya 1,000 kiwango cha joto kwa kutumia vifaa maalum vya 'themoscan'.

Hivi karibuni, Bazara la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), lilieleza kwamba kuna maelekezo yametolewa kwa kanisa hilo, duniani ambayo yatatekelezwa na makanisa kwa kuzingatia hali katika nchi husika na kwamba nchini mikusanyiko ya ibada bado haijakatazwa na kwamba wanachukua tahadhari kukabiliana na kusambaa kwa corona.

Katika mwongozo uliotolewa, Alhamisi Kuu hakutakuwa na kuoshwa miguu wala maandamano ya Ekaristi Takatifu na badala yake Sakramenti Takatifu itahifadhiwa katika tabernako.

Mwongozo mwingine ni kwamba hakutakuwa na utaratibu wa kubusu msalaba na badala yake waumini watainamia msalaba kwa mbali bila kuugusa wala kuushika.

Jingine ni kusitishwa kuwekwa maji ya baraka ya kuchovya katika milango, na waumini hawatakiwi kupeana mikono badala yake wafumbe mikono na kuinamiana kwa heshima, na kwamba waumini watakominika kwa mikono tu.

Mwingine ni kila muumini kutumia kitabu chake cha ibada na wanaohesabu fedha za matoleo watumia vitakasa mikono (maji tiba) kujisafisha.

Nyingine ni sakramenti ya kitubio, Padri anayeungamisha asiangaliane na waumini uso kwa uso katika kiti cha kitubio bali maungamo yafanyike sehemu za wazi.

Habari Kubwa