KLM yarejesha safari, ndege yake yatua na watalii 117 KIA

06Aug 2020
Allan lsack
Hai
Nipashe
KLM yarejesha safari, ndege yake yatua na watalii 117 KIA

SHIRIKA la Ndege la Kimataifa la Uholanzi (Royal Dutch Airlines - KLM), limerejesha tena huduma zake nchini, baada ya juzi ndege yake kutua na watalii 117 ikiwa miezi minne tangu liliposimamisha huduma kutokana na baa la corona.

Juzi, shirika hilo lilizindua kurejea kwa huduma zake nchini baada ya kushuka kwa ndege yake ya abiria yenye namba za usajili Boeing 777 PH-BQB katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Jana, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk. Anna Mghwira, akizungumza na waandishi wa habari baada ya mapokezi ya ndege hiyo, alisema kuingia kwa watalii hao nchini kunaidhihirishia dunia kuhusu ushindi dhidi ya virusi vya corona.

“Kuja kwa watalii hawa ni ishara ya ushindi mkubwa, ni ishara njema ya amani na upendo, hivyo ninawaomba wananchi popote walipo watambue kuwa Tanzania ni sehemu salama ya utalii," alisema Mghwira.

Watalii hao waliotokea mataifa mbalimbali ya Bara la Ulaya na Asia, wako nchini kwa ajili ya kutembelea vivutio vya utalii, hasa hifadhi za taifa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), vilivyoko Kaskazini mwa Tanzania.

Awali, mashirika ya ndege ya kimataifa yalisitisha safari zake kwenye nchi mbalimbali duniani kutokana na tishio la maambukizi ya virusi vya corona.

Mashirika ya ndege ambayo hadi sasa yamesharudisha safari zake nchini, ni pamoja na RwandAir, Ethiopia, Qatar, Emirates na KLM.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa mkoa, kurejea kwa safari za ndege hizo, kumeithibitishia dunia kwamba wananchi wa Tanzania wameishinda hofu ya ugonjwa huo.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Usimamizi na Uendeshaji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KADCO), Christine Mwakatobe, ndege hiyo ya KLM iliwasili saa 2:15 usiku wa Agosti 4 mwaka huu ikiwa na watalii kutoka Ujerumani, Uingereza, Ufaransa na wengine wa Bara la Asia.

Alisema kurejea kwa safari za ndege kumetokana na serikali ya Uholanzi kuridhika na jitihada za Serikali ya Tanzania katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa corona.

Agosti 2 mwaka huu, Mkoa wa Kilimanjaro uliipokea ndege nyingine ya Shirika la Ndege la Rwanda (RwandAir) yenye usajili wa namba 9XR- WL.

Juni Mosi mwaka huu, walipokea ndege ya Shirika la Ethiopia na Julai 30 walipokea ndege ya Shirika la Qatar, na Agosti Mosi mwaka huu, walipokea ndege ya Crystal P4_XTL.

Akizungumza kwa niaba ya watalii wenzake waliokuja kutembelea hifadhi za taifa nchini, Getrude Boldemann, raia wa Ujerumani, alisema wamefurahishwa sana na kauli ya Rais John Magufuli kwamba Tanzani hakuna ugonjwa wa corona, ndiyo sababu wamekuja kutalii kwenye mbuga za wanyama.

Habari Kubwa