Kofia ya CCM kumtenga Magufuli na wananchi?

02Mar 2016
Na Waandishi Wetu
Dar
Nipashe
Kofia ya CCM kumtenga Magufuli na wananchi?
  • ******Wasomi wasema ana kibarua kizito kuushinda mtihani huo.

IKIWA imesalia miezi mitatu sasa Rais John Magufuli akabidhiwe uongozi wa CCM, madaraka hayo mapya kuwa mtego kwa kiongozi huyo mkuu wa nchi na kwamba yataweza kupunguza au kuongeza kukubalika kwake kwa wananchi.

Mwenyekiti wa CCM Dk. Jakaya Kikwete na Rais Dk. John Pombe Magufuli.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema kiongozi huyo atakuwa mtegoni baada ya kukabidhiwa wadhifa huo na kwamba baadhi ya watu wanaomuunga mkono kwa sasa, wengine wakiwa si wapenzi wa CCM na wengine ni wapenzi, watatofautiana naye.

Kwa miaka ya karibuni, imekuwa desturi kwa viongozi wa CCM kuachiana madaraka kabla ya uchaguzi mkuu wa chama, tofauti na Mwalimu Julius Nyerere ambaye alimwachia Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, uongozi wa chama baada ya miaka mitano. Nyerere alimkabidhi Mwinyi kijiti cha uenyekiti wa CCM mwaka 1990, wakati alianza kuwa Rais mwaka 1985.

Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, alikabidhiwa chama na Mwinyi mwaka 1996 ikiwa takribani miezi saba baada ya kuchaguliwa, huku naye akimkabidhi Jakaya Kikwete Juni 2006, ikiwa miezi sita, baada ya kuchaguliwa kuiongoza Tanzania.

Kama ilivyokuwa kwa Kikwete, inatarajiwa kuwa Juni, mwaka huu, CCM itafanya Mkuu Mkuu Maalumu wa Taifa, ambao pamoja na mambo mengine, utamchagua mwenyekiti wake wa taifa, ambaye bila shaka atakuwa Rais Magufuli.
Kukabidhiwa kwake chama, kutamfanya asimame si tu kama Rais wa nchi, bali pia Mwenyekiti wa CCM, chama cha siasa chenye misimamo yake ambayo baadhi inapingwa na wale wasio wapenzi pamoja na makada wa chama hicho.

KATIBA MPYA
Mtihani wa kwanza unaotajwa kumkabili Rais Magufuli, ni suala la Katiba Mpya, ambalo si tu lina ukinzani nje ya CCM bali hata ndani ya chama hicho kikongwe limegawa wanachama wake.

Baadhi ya watu wasiokubaliana na Katiba Inayopendekezwa ni pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, ambaye kwenye uchaguzi mkuu uliopita, alikuwa mmoja wa watu waliokuwa mstari wa mbele kumpigia Rais Magufuli kampeni.

Kutokana na hali hiyo, ni wazi kwamba Rais Magufuli atakapopokea kijiti kuwa Mwenyekiti wa CCM, akiamua kuendelea na Katiba Inayopendekezwa, atakuwa tofauti na Jaji Warioba na wengine waliokuwa wakipinga akiwamo Joseph Butiku, kada mwingine wa CCM aliyekuwa akijitokeza hadharani kuipinga.

Mbali na makada hao ambao ni sehemu ya kundi lililomwingiza Rais Magufuli madarakani kwa kumpigia kampeni majukwaani, pia kuna kundi lingine kubwa la watu ambao si waamini wa CCM na wanaipinga Katiba Inayopendekezwa, ingawa sasa wanamuunga mkono Rais Magufuli kwa utendaji wake.

Kwa mantiki hiyo, baada ya Magufuli kukabidhiwa chama, akiamua kusimama na Katiba Inayopendekezwa, kuna kundi kubwa ambalo litajitenga naye na vivyo hivyo akiamua kurudi nyuma ili kuridhisha kundi hili, atakuwa na wakati mgumu ndani ya chama kwa wale wanaoikubali Katiba hiyo ambayo kwa sasa inasubiri kupigiwa kura ya maoni.

Alipokuwa akifungua Bunge la 11, Novemba 20, mwaka jana, Rais Magufuli alizungumzia kwa ufupi juu ya Katiba Mpya. Hata hivyo, kwa maelezo yake ni vigumu kutafsiri moja kwa moja na kujua msimamo wake.

Katika maelezo yake alisema, “Serikali yangu imepokea kiporo cha mchakato wa Katiba ambao haukuweza kukamilika katika awamu iliyopita kutokana na kutokamilika kwa wakati kwa uandikishaji wa wapigakura.

“Napenda kuwahakikishia kuwa tunatambua na kuthamini kazi kubwa ya kizalendo iliyofanywa na wananchi walioshiriki hatua ya awali ya ukusanyaji wa maoni kuhusu Katiba mpya. Tume ya Marekebisho ya Katiba na Bunge la Katiba lililotupatia Katiba Inayopendekezwa. Tutatekeleza wajibu wetu kama ulivyoainishwa katika Sheria ya Marekebisho ya Katiba.”

HALI YA KISIASA YA ZANZIBAR
Hali ya kisiasa ya Zanzibar kwa miaka mitano ijayo ni moja ya mambo ambayo yatapima utendaji wa Rais Magufuli akiwa Amiri Jeshi Mkuu, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, chama chenye upinzani mkubwa visiwani huko pamoja na kile cha CUF.

Licha ya kwamba Magufuli ametoa msimamo wake juu ya suala la Zanzibar, na kusema hawezi kuingilia lolote akisema mambo yote yako chini ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec), baada ya uchaguzi wa marudio, atakuwa na kazi ya kuunganisha wafuasi wa chama chake na wale wa CUF.

ZEC imetangaza kwamba uchaguzi wa marudio visiwani humo utakuwa Machi 20, lakini bado wachambuzi wa siasa wanasema miaka mitano ijayo hakutakuwa na hali nzuri ya kisiasa katika sehemu hiyo ya Tanzania.

Wachambuzi hao wanasema miaka mitano iliyopita, hali ya kisiasa visiwani humo ilionekana tulivu kwa sababu tu, chama kikuu cha upinzani visiwani humo, CUF, kilishirikishwa katika kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kama ambavyo Katiba ya Zanzibar inataka chama kitakachopata zaidi ya asilimia 10 kwenye uchaguzi, kitajumuishwa kwenye serikali.

Kwa maelezo yao, baadhi ya wananchi wa Zanzibar, hasa wale wapenzi wa CUF, wanasema wanarudi kwenye zama za uhasama ambazo watu walikuwa hawauziani vitu dukani, hawasalimiani na mbaya zaidi hata hawazikani.

Hivyo litakuwa jukumu la Rais Magufuli kuhakikisha anatumia nafasi yake ya Rais na Mwenyekiti wa CCM, kuunganisha wananchi na wanachama wa chama chake na kile cha upinzani ili kuchochea maendeleo katika visiwa hivyo.

WATUHUMIWA NDANI YA CCM
Tangu aingie madarakani, Rais Magufuli na wasaidizi wake wamesimamisha na kufukuza zaidi ya watumishi wa umma 160 kwa tuhuma mbalimbali, zikiwamo za rushwa, ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.

Wakati akifanya hayo, kwa muda mrefu ndani ya chama chake, kumekuwa na makada wanaotuhumiwa kwa rushwa na mambo mengine yanayogharimu rasilimali za nchi.

Tuhuma hizo zilifanya chama hicho kifike mahali kuibuka na kaulimbiu ya ‘kujivua gamba’, jambo ambalo baadaye lilifutika kimya kimya.

Kwa hiyo akiwa Mwenyekiti wa CCM, walio wengi watampima Rais Magufuli kama kweli ataweza kuwachukulia hatua watu hao ambao wanaaminika kuwa vigogo ndani ya chama chake au atawakumbatia, ambao waliwahi kukumbwa na kashfa mbalimbali za ufisadi.

MAKUNDI NDANI YA CCM
Makundi ni jambo lingine ambalo limekuwa sehemu ya CCM na kwa miaka mingi licha ya kujinadi kwamba makundi huvunjwa baada ya uchaguzi lakini mara nyingi huibuka kila inapiotokea uchaguzi.

Baadhi ya wachambuzi wanasema kwa awamu hii jambo hilo linaweza lisionekane sana ndani ya chama kwa sababu Magufuli hakuwa na kundi kubwa ndani ya CCM, ingawa wengine wanasema hata sasa makundi ya uchaguzi wa 2015 bado yapo na hayafikiriwi kuvunjika.

Kinachoonyesha kwamba mpaka sasa makundi hayo bado yapo, ni kauli mbalimbali ambazo zimekuwa zikitolewa na baadhi ya makada wa chama hicho tangu kumalizika kwa uchaguzi ndani ya chama na hatimaye uchaguzi mkuu.

Pia kauli aliyoitoa Magufuli mwenyewe baada ya kutangazwa mshindi katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana pamoja na ile ya mwenyekiti wa chama hicho, Kikwete, aliyoitoa hivi karibuni kwamba kuna watu walikisaliti chama, zinaonyesha bado makundi yapo mengi.

Kwa maana hiyo, Rais Magufuli atakuwa na kazi ya kuyaunganisha makundi hayo, jambo ambalo linaweza kuleta mpasuko zaidi au kukiunganisha chama kulingana na njia atakayotumia.

STAILI YAKE YA UONGOZI
Rais Magufuli anaelezwa ni kiongozi mtendaji na mwenye amri anayetaka matokeo na si mwanasiasa, ndiyo maana tangu akiwa waziri amekuwa mtu wa kutoa matamko na kuchukua hatua.

Mfumo wake huo unaoelezwa kuwa mzuri kwenye utendaji wa serikali wakati kwenye uongozi wa chama cha siasa, hali ni tofauti. Mambo mengi huendeshwa kwa majadiliano, kujenga hoja za kisiasa ili kushawishi watu wengine waridhie kile kinachotakiwa.

Katika hili pia, walio wengi hasa waliokuwa wapinzani wake wakati wa kutafuta mgombea wa kupeperusha bendera ya chama hicho, walidai Magufuli hakijui chama kwa sababu hajawahi kuwa kiongozi kwenye ngazi yoyote ya chama hicho zaidi ya kuwa mjumbe wa mkutano mkuu kwa mwamvuli wa ubunge.

Ingawa hoja hiyo inaweza isiwe na mashiko kwani amekuwa mbunge tangu mwaka 1995 na kupata nafasi ya kuhudhuria vikao mbalimbali vya chama kuanzia ngazi ya wilaya hadi taifa.

Hata hivyo, wale waliotoa madai hayo hawatasita kumpima kiongozi huyo pale atakaposhika hatamu za kuongoza CCM.
Baadhi ya wachambuzi wanashauri ikiwa Rais Magufuli atashika wadhifa huo mzito wa kuongoza chama atapaswa kuwa mwanadiplomasia zaidi.

KUTENGANISHA SIASA NA BIASHARA
Suala la kutenganisha biashara na siasa limekuwa likizua mijadala kwa miaka mingi bila kupatiwa ufumbuzi na matokeo yake limeishia kujadiliwa kwenye majukwaa.

Wakati ya serikali ya awamu ya nne, suala hili lilielezwa kuwa lilikuwa kwenye mchakato wa kuandaliwa rasimu lakini likayeyuka.

Kikubwa kilichokuwa likisukuma mjadala huu, ni Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma inayodaiwa kuwa na upungufu, ukiwamo ule unaofanya matamko yanayotolewa na viongozi hao kuwa siri na kwamba atakayetoa siri hiyo anahesabika amefanya kosa la jinai.

Rais Magufuli, tangu aingie madarakani, amejitahidi kuwa mbali na wafanyabiashara, huku akisema hata kwenye kampeni zake hakuchangiwa hata senti moja na kundi la watu hao.

Kauli zake hizo zinategemewa kuonekana pia kwenye chama kwamba baadhi ya wafanyabiashara hawatakuwa sehemu ya kuendesha siasa za chama na nchi kwa ujumla.

RUSHWA KUPATA UONGOZI
Jambo lingine ambalo limeonekana ni mtihani hasa ndani ya CCM ni viongozi wake kupata nafasi walizo nazo kwa kutumia fedha.

Baadhi ya viongozi ndani ya CCM wamekuwa wakilalamika juu ya matumizi makubwa ya fedha kusaka uongozi ndani ya CCM na vyombo vya uamizi kama urais, ubunge na udiwani.

Mwaka 2007, kwa mfano, Kikwete alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa CCM kwenye ukumbi wa Kizota, Dodoma, alionyesha kushangazwa na matumizi makubwa ya fedha kwa wanachama na makada waliokuwa wakiomba ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho.

Baadhi ya makada waliokuwa wanasaka nafasi hizo, walibuni mbinu mbalimbali za kutafuta kura ikiwa pamoja na kuwafuata wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM kwenye mikoa yao na hata kutumia wapambe wao kusafiri na kutoka mikoani huko hadi Dodoma.

Mbali na mbinu hiyo, makada hao walikuwa wakiwaingizia fedha baadhi ya wajumbe kwenye akaunti zao au kwenye simu kwa mtindo wa muda wa mazungumzo.

Hata katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 na ule wa mwaka jana, madai ya kuwapo matumizi makubwa ya fedha kusaka urais, udiwani na ubunge yalielezewa kutamalaki katika sehemu mbalimbali nchini.

Kutokana na hali hiyo, wakati yeye (Rais Magufuli) akijipambanua kuwa kinara wa kupambana na rushwa wakati chama chake kimekuwa kikihusishwa na watu wanaotumia fedha ili kupata nafasi mbalimbali za uongozi.

Ni wazi kwamba uongozi wake ndani ya chama hicho, utaangaliwa pia kwa namna ambavyo kiongozi huyo atapambana na picha hiyo mbaya ya chama chake.

WASOMI WAZUNGUMZA
Mwanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Kitilla Mkumbo, alisema Rais Dk. Magufuli ana mtihani mkubwa katika kukisafisha chama pindi atakapokabidhiwa rasmi.

Alisema suala la kuchanganya biashara binafsi na siasa ndani ya CCM limeota mizizi kwa sababu hata mwaka 2005 Rais mstaafu Jakaya Kikwete alipoingia madarakani alitangaza kupambana nalo lakini alishindwa.

“Suala la kukataza kuchanganya biashara na siasa halipo katika ilani ya CCM lakini ni jambo ambalo limeota mizizi, hivyo Rais Magufuli ana kazi kubwa ya kuliondoa,” alisema.

Alisema suala la Katiba mpya nalo halikuwapo katika ilani ya CCM bali ilikuwa utashi wa Rais mstaafu Kikwete, hivyo linapaswa kuangaliwa kwa upana zaidi.

Alisema Rais Magufuli kumalizia suala la Katiba mpya, kama wananchi wanavyotaka, ni kujipa matumani hewa kwa sababu mchakato huo unaendeshwa na viongozi wababe ndani ya CCM wanaotaka maslahi yao binafsi.

Kuhusu kuwapo kwa makundi ndani ya CCM, Profesa Mkumbo alisema makundi hujitokeza wakati wa uchaguzi tu, alisema kwa sasa makundi hayo yameshavunjika na yanaweza kujitokeza katika ucahaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Aliongeza kuwa Rais Magufuli ana mamlaka ya kumfukuza mtumishi wa serikali au kumsimamisha wakati wowote lakini hana mamlaka ya kumfukuza mwananchama mpaka Kamati Kuu ifanye vikao na kuamua.

Kuhusu mgogoro wa Zanzibar, alisema si mgeni kwa kuwa ulikuwapo tangu mwaka 1995, hivyo ni mgogoro utakaoendelea endapo vyama vya siasa vya CCM na CUF havitakubalina.

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa na Utawala wa UDSM, Dk. Bashiru Ally, alisema ndani ya CCM kuna makundi mbalimbali yakiwapo CCM Maslahi, CCM Mtandao, CCM Waasisi na CCM Wafadhili.

Alisema tangu kuanzishwa kwa CCM mwaka 1977, chama hicho kilibadilika kutoka chama cha ukombozi hadi kuwa chama cha kupigania madaraka au uongozi.

Alisema kwa sasa vyama vya siasa nchini vimekuwa chonganishi kwa wananchi ili wavipigie kura. Alisema staili vinayotumia kuwachonganisha ni kwa kutumia maeneo, ukabila na udini.

Kuhusu Katiba Mpya, Dk. Ally alisema mchakato huo ulivamiwa na wanasiasa uchwara, hivyo Rais Dk. Magufuli ana kazi kubwa ya kuhakikisha unawaridhisha wananchi.

Pia alisema Rais Magufuli anapaswa kukirudisha chama mikononi mwa wananchi na kubadilisha mtindo wa siasa uliosababisha mchakato kukwama.

Kuhusu makundi, alisema Rais. Dk. Magufuli anapaswa kuwa na kauli ndani ya chama vinginevyo makundi hayatamalizika.
Alisema Rais Magufuli ili aweze kukisafisha chama, anatakiwa kuanzisha mahakama ya kusikiliza kesi za ufisadi kwa kuwa baadhi ya makada wake wanatuhumiwa kujihusisha na rushwa, ufisadi na ujangili.

Alisema kiongozi wa chama kuhusishwa na vitendo vya ufisadi na ujangili ni kosa, hivyo wanapaswa kuchunguza na kuchukuliwa hatua.

Naye mwanazuoni mkongwe wa siasa na mwanataaluma wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (Saut), Profesa Mwesiga Baregu, alisema Rais Magufuli anakabiliwa na changamoto pindi atakapokabidhiwa chama kwa sababu hana mizizi, hivyo anaweza asipate ushirikiano kwa wananchama na viongozi walioni ndani ya CCm.

Alisema Rais Magufuli kama anataka kukibadili chama, akubali kukabiliana na upinzani mkubwa, hivyo itategemea atakuwa na utayari wa namna gani.

“Ukizangatia Rais Magufuli hakupewa nafasi kubwa kushinda tiketi ya urais wa nchi kupitia CCM, hiyo itampa wakati mgumu wa kukisafisha chama,” alisema Profesa Baregu.

Kuhusu Katiba Mpya, Profesa Baregu alisema Rais Magufuli atakuwa na wakati mgumu kwa sababu endapo ataendelea pale ulipoishia atakuwa amefanya kosa kubwa.

Mwanazuoni mwingine, Profesa Ernest Mallya, alisema katika taasisi yoyote kuna makundi, hivyo hata katika siasa kuna makundi mengi.

“Apende asipende Rais Magufuli makundi katika vyama yatakuwapo tu, lakini anachotakiwa ni kuhakikisha anakuwa mwangalifu,” alisema Profesa Mallya, ambaye ni mwanataaluma wa UDSM katika Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala.
Alisema kuhusu biashara na siasa, Rais Magufuli anachotakiwa ni kuhakikisha kunakuwapo na uwazi ili viongozi wasifiche mali zao.

Kwa upande wa rushwa, alisema Rais Magufuli kuondoa rushwa ndani ya CCM ni ngumu kwa sababu CCM imeonyesha wazi kuwa inalea rushwa. Alisema hiyo ilitokea wakati wa kura za maoni huku wakubwa na wadogo wakishindana kutoa.

Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya siasa nchini, Abdulhakim Atiki, alisema pindi Rais Dk. Magfuli atakapokabidhiwa chama kukiongoza, atatakiwa kuwa makini kwa sababu badala ya kusafisha anaweza akawa anakiharibu kabisa.

Alisema chama chochote cha siasa hata ambacho kina mlengo wa kushoto, hakiwezi kukosa wanachama ambao wanakuwa na mlengo wa kulia.

Alisema Rais Magufuli atatakiwa kuwa makini kwa kufuata ilani ya chama pekee.

Habari Kubwa