Komandoo mwingine adai kuteswa polisi

02Dec 2021
Kulwa Mzee
Dar es Salaam
Nipashe
Komandoo mwingine adai kuteswa polisi

KOMANDOO Gabriel Mhina amedai alikamatwa mkoani Tabora, alisulubiwa na kupigwa kwa saa tatu na askari polisi, akitakiwa kueleza uhusiano alionao na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe.

Amedai kuwa baada ya kukataa kuwa na uhusiano na kiongozi huyo, aliteswa zaidi.

Shahidi huyo wa tatu upande wa utetezi alikuwa mshtakiwa kwenye kesi ya ugaidi, akaachiwa baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuwasilisha hati ya kuwaondoa kwenye kesi pamoja na wenzake wawili Julai 27, mwaka huu.

Amiri alidai hayo jana Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi mbele ya Jaji Joackim Tiganga wakati akitoa ushahidi upande wa utetezi kwenye kesi ndogo ndani ya kesi kubwa ya ugaidi.

Akiongozwa na Wakili Dickson Matata, alidai Septemba 19, mwaka 2020, alipigiwa simu na rafiki yake anayeitwa Dida wakaangalie mpira Oxygen Pub, maeneo ya Makokora mkoani Tabora.

Shahidi huyo alidai akiwa eneo hilo, ghafla alikamatwa na askari wa kikosi maalum, mmoja akimtolea bastola na kumfahamisha anahitajika kwa RCO.

"Nilikubali kupanda gari lao, Toyota Land Cruiser jeusi, kwenye gari nilikuwa mimi na wao watatu, nilikaa mbele na dereva hadi Kituo cha Polisi Tabora.

"Wakati ninasubiri kuonana na RCO walinifunga pingu wakanipeleka ndani ya kituo nyuma, waliniuliza 'kesho kuna tukio gani?' Nikasema kuna ujio wa Rais Magufuli, anakuja kufanya kampeni.

"Kule nyuma walinihoji nina uhusiano gani na Mheshimiwa Mbowe huku wakinipiga vibaya kila sehemu ya mwili wangu, walinipiga kwa kutumia fimbo, ngumi kwenye taya na mateke.

"Alikuwa Goodluck, kiongozi wao alikuwa afande Jumanne, kulikuwa na Minja na afande Aziz, mmoja simkumbuki.

"Nilipigwa kwa saa tatu, nilipokuwa nakataa kuwa na uhusiano na Mbowe walinipiga zaidi, wakanipeleka Kituo cha Polisi cha Reli Tabora maana hali yangu ilikuwa mbaya," alidai Mhina.

Alidai kuwa wote waliokuwa wanamsulubu ndio waliompeleka Kituo cha Reli na kumfuata siku iliyofuata Septemba 20, 2020 saa nne asubuhi.

Shahidi alidai walimuuliza kuhusu mshtakiwa wa tatu Mohammed Ling'wenya kama anamfahamu, alikiri anamfahamu na aliwahi kufanya kazi naye Kikosi cha Makomandoo 92 KJ Ngerengere na alipotoka kazini alikuwa rafiki yake wa karibu.

Alidai kuwa asubuhi saa tano, alipelekwa Nzega akiwa amefungwa pingu na kafungwa kitambaa usoni, walipomfikisha Kituo cha Polisi Nzega walimwacha na hakujua walikokwenda.

"Walirudi siku ya pili wakiwa na Malema ambaye alishawahi kuwa komandoo. Nilimfahamu komandoo kwa sababu mazingira yake ya kukamatwa yalikuwa kama yangu.

"Nilimuuliza alisema alikuwa komandoo, siku inayofuata tulianza safari ya kupelekwa Dar es Salaam, kila mtu na gari lake," alidai Mhina.

Alidai kuwa walipotoka Nzega, walifikishwa Kituo cha Polisi Tazara, mahabusu na askari walimfahamisha palikuwa Tazara.

Shahidi huyo alidai alifika Tazara Septemba 23, 2020, akakaa siku mbili na ilipofika Septemba 25 alifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kushtakiwa kwa tuhuma za ugaidi.

Alidai kuwa akiwa Tazara, mahojiano yalikuwa yakifanyika juu kulikokuwa na chumba, alidai Malema alihojiwa na Inspekta Mahita Omari na yeye alihojiwa na SP Jumanne.

Shahidi huyo alidai aliambiwa ataunganishwa na wenzake kwenye kesi ya ugaidi namba 63/2020 na kwamba akiwa Tazara, alikuwa anakunywa maji tu, chakula alikula Septemba 25 gerezani baada ya kutoka mahakamani.

"Julai 27, mwaka huu, tulipofika mahakamani, Hakimu Thomas Simba alisema serikali haina nia ya kuendelea na shauri letu, nikaachiwa mimi, Kaaya na Khalid.

"Tukiwa gerezani Ling'wenya alinifahamisha mateso yote aliyokuwa akiyapata tangu Moshi alipokamatwa hadi Dar es Salaam," alidai Mhina.

Awali shahidi wa pili wa utetezi katika kesi ndogo, Lembrus Mchome aliomba mahakama hiyo kutenda haki kwenye kuendesha kesi ya ugaidi inayomkabili Mbowe na wenzake watatu.

Akihojiwa na Wakili Fredrick Kihwelo aliyetaka kujua shahidi alikuwa na maana gani alipokuwa akizungumza michango kwenye tweet zake, alidai alikuwa anamaanisha baadhi ya mashahidi wanaoletwa mahakamani sio wa kweli na mashtaka ni ya kutungwa.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Mbowe, Adamu Kasekwa, Ling'wenya na Halfani Bwire ambao wanatuhumiwa kwa mashtaka sita yakiwamo kula njama kufanya vitendo vya kigaidi kati ya Mei Mosi na Agosti 5, mwaka 2020.

Habari Kubwa