Komba atoa mbinu kwa wanawake watia nia kushinda uchaguzi 

25Jun 2020
Dotto Lameck
Tanga
Nipashe
Komba atoa mbinu kwa wanawake watia nia kushinda uchaguzi 

MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga kupitia Chadema, Yosepher Komba, ametoa mbinu za kupata ushindi kwa wanawake wanaotia nia kuwania nafasi za uongozi katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Mwezi Oktoba, mwaka huu.

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga, Yosepher Komba akizungumza na washiriki wa semina maalumu kwa wanawake mkoani humo.

Komba ametoa mbinu hizo katika semina maalumu iliyoandaliwa na Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Wanawake na Uongozi, huku akisema kuna umuhimu wa wao kuzingatia dhamira ya dhati katika kugombea nafasi ya uongozi.  

Komba amesema mbinu zinazotakiwa kuzingatiwa katika harakati za kisiasa kupata mafanikio ni kuwa na rasilimali watu, muda, fedha na taarifa ya eneo husika.

Baadhi ya washiriki waliohudhuria semina hiyo.

“Ndugu zangu hizo ni mbinu muhimu sana hasa unapotaka kusaka uongozi wa kisiasa hivyo tambueni rasilimali watu mnapaswa kulipa kipaumbele sana kwani ndio silaha ya ushindi na kuweza kuwafikisha kwenye mahali mnapotaka” amesema Komba.

Aidha, Komba amewataka wanasiasa wanawake mkoani Tanga kujiamini na kuchukua hatua pindi wanapojitokeza kuomba kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ili kufanikisha ndoto zao wa kuwatumikia wananchi katika maeneo mbalimbali.

Semina hiyo ilishirikisha wajumbe wanawake kutoka katika vyama vitano vyenye uwakilishi ambavyo ni Chadema, CCM, NCCR Mageuzi, ACT na Chama cha Wananchi.

Habari Kubwa