Kongamano la wadau wa sera za kilimo kufanyika kesho Dodoma

11Feb 2020
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Kongamano la wadau wa sera za kilimo kufanyika kesho Dodoma

Kongamano la sita la wadau wa sera za kilimo(AAPC), linatarajiwa kufanyika kwa siku tatu jijini Dodoma, likiwa na lengo la kujadili masuala mbalimbali ya kisera ikiwemo mnyororo wa kuongeza thamani na usalama wa chakula nchini.
 

Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la wadau wa kilimo wasio wa kiserikali (ANSAF), Audax Rukonge.

Mkutano huo utaanza Februari 12-14, mwaka huu na utakuwa na washiriki zaidi ya 250 ikiwemo wasomi, taasisi za utafiti, watunga sera, vikundi vya utetezi na watendaji wa serikali.

Akizungumza leo na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la wadau wa kilimo wasio wa kiserikali (ANSAF), Audax Rukonge, amesema kongamano hilo litakusanya wadau wa sekta binafsi na umma na litajikita katika maeneo saba ambayo ni sera ya kilimo, biashara na uwekezaji, uzalishaji katika sekta binafsi.

Pia amesema litajadili upatikanaji wa pembejeo na matumizi yake, upatikanaji wa fedha na huduma saidizi, ardhi, maliasili na mazingira pamoja na usalama wa chakula na lishe.

“Tutajadili kwa kina masuala haya saba kwa kuwa idadi ya watu duniani inaongezeka Tanzania na barani Afrika kwa ujumla, ambapo Tanzania ni asilimia 2.8 kwa mwaka huku uchumi ukikua kwa asilimia 7 kwa mwaka, kumekuwa na hoja nyingi kwanini uchumi unakua lakini watu ni maskini,”amesema.

Mkurugenzi huyo amesema kinachoonekana ni sekta zinazogusa watu wengi hazikui kwa kiwango kinachotakiwa kama uchumi unavyokua.

“Sekta ya kilimo ambayo inategemewa na wananchi wengi haikui kwa kiwango kinachotakiwa na ngazi ya uzalishaji ipo chini, kilimo bado hakijamwezesha mtu ajitegemee,”amesema.

Aidha, amesema uchakataji wa bidhaa bado ni mdogo na viwanda vilivyopo vinategemea asilimia 65 ya mazao yanayotokana na sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Amebainisha washirika wengine wakuu wa maendeleo ambao watakuwepo katika mkutano huo ni viongozi wa Serikali, REPOA, Benki ya Dunia, FAO na UN Women.

“AAPC imefadhiliwa na USAID, FAO, Benki ya Dunia, TADB, UN Women, JICA, AGRA, ASPIRES, TAHA, Dalberg na FSDT, tunatumai kuwa mwishoni mwa mkutano huo wadau wa kilimo watapewa nguvu na zana sahihi ili kufanya mabadiliko muhimu kwa upanuzi wa sekta na maendeleo ,”amesema

Habari Kubwa