Korti yaamuru Mbowe kukamatwa

09Nov 2018
Hellen Mwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Korti yaamuru Mbowe kukamatwa

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imetoa hati ya kukamatwa kwa Mwenyekiti Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko, kujieleza kwanini wasifutiwe dhamana kwa kushindwa kufika kusikiliza kesi yao.

Mwenyekiti Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe.

Mbowe, Matiku pamoja na viongozi wengine wa Chadema  wanakabiliwa na kesi ya uchochezi.

Amri hiyo ilitokana na jopo la Mawakili wa Jamhuri likiongozwa na Mawakili wa Serikali Wakuu, Faraja Nchimbi, Dk. Zainabu Mango na Wakili wa Serikali Jackline Nyantori, kuomba mahakama kutoa hati ya kukamatwa washtakiwa hao.

Maombi hayo yaliwasilishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.

Hakimu alisema taarifa za mdhamini wa mshtakiwa Mbowe zinajichanganya na kudai kuwa Novemba Mosi, mwaka huu, mdhamini alidai mahakamani kuwa mshtakiwa yuko mahututi  amepelekwa kwenye matibabu Afrika Kusini na mahakama ilimwamini na akaahidi kupeleka vielelezo.

"Mahakama ilimwamini mdhamini kwamba ataleta vielelezo vya matibabu ya Mbowe, lakini leo (jana), anasema amekwenda kutibiwa Dubai, inaonyesha wazi mdhamini si mwaminifu, mshtakiwa Matiko anakosa kuhudhuria kesi yake mara kwa mara na amesafiri nje ya nchi bila kibali cha mahakama, anatumia vibaya haki yake ya kikatiba ya dhamana," alisema hakimu wakati akitoa amri dhidi ya washtakiwa hao.

Alisema kesi hiyo itaendelea kusikilizwa ushahidi wa Jamhuri Novemba 22, mwaka huu.

Awali, mahakama hiyo iliwaamuru vigogo saba kati ya tisa waliofika kusikiliza kesi hiyo akiwamo Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa na wenzake kuacha kuidharau, kumkaripia hakimu ama kuigeuza kama ukumbi wa Bunge kwa kuwa ni washtakiwa kama wengine.

Kadhalika, mahakama hiyo imesema haiwatambui wao kama vigogo wa Chadema na kuwataka waheshimu mamlaka halali ya mhimili huo kama washtakiwa na si vinginevyo.

Hakimu alitoa amri hiyo baada ya washtakiwa hao kugoma kukubali au kukataa walipokumbushwa mashtaka yao pamoja kusomewa maelezo ya awali bila kuwapo Wakili wa Utetezi, Peter Kibatala, baada ya kushikiwa mikoba na Wakili John Mallya kwa madai kuwa ni mgonjwa.

Hakimu alisema washtakiwa wote wanajua sheria za nchi na kwamba wanaichezea haki yao ya msingi.

"Uandike kama nilivyosema nasubiri uwepo wa wakili wangu, umesikia? Uandike kama nilivyosema," alidai Mdee na kusababisha hakimu kumjia juu na kumwamuru asirudie tena kumkaripia.

"Mko hapa kama washtakiwa na si wabunge wala vigogo wa Chadema, nawaheshimu sana kama washtakiwa wengine wanaposimama mbele yangu, sitaki mwendelee kunidharau, mshtakiwa wa saba Halima Mdee usinikaripie na usirudie tena kunikaripia nasisitiza tena usinikaripie," alisema na kuongeza:

"Kila mtu anajua sheria za nchi hii hasa nyie washtakiwa wote ninapokaa hapa mimi kama hakimu na ninyi hapo kizimbani kama washtakiwa," alisema.

Mapema jana upande wa Jamhuri ulidai kuwa uko tayari kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali bila uwepo wa wakili wa utetezi kwa sababu moja kwa moja wanajibu washtakiwa wenyewe.

Nchimbi alidai kuwa kabla ya kusomewa maelezo hayo washtakiwa watakumbushwa mashtaka yanayowakabili.

Aidha, kutokana na Kibatala kuwa mgonjwa, washtakiwa sita waliomba kesi hiyo isikilizwe kwa sababu ni haki yao kuwakilishwa.

Wakili Jamhuri Johnson, aliyekuwa anamtetea Msigwa alipinga maelezo ya awali yasisikilizwe kwa sababu mshtakiwa wa kwanza na wa tano hawakuwapo mahakamani.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, mahakama ilisema ombi la Jamhuri limekubaliwa na washtakiwa wakumbushwe mashtaka yao na wasomewe maelezo ya awali.

Washtakiwa walipokumbushwa mashtaka yao, Msigwa alikana, lakini wenzake walidai kuwa hawawezi kujibu chochote bila kuwa na wakili wa kuwawakilisha.

Baada ya hakimu kuruhusu maelezo ya awali kusomwa, Wakili  wa Jamhuri alijitoa kumwakilisha Msigwa.

"Mheshimiwa najitoa kumtetea mshtakiwa wa pili, Msigwa siwezi kuendelea na kesi hii," alidai Jamhuri.

Akiwasomea maelezo ya awali, Dk. Mango, alidai Februari, mwaka huu kulikuwa na uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kinondoni na vyama 12 vilishiriki kikiwamo Chadema.Alidai vyama vyote vilipaswa kuheshimu na kufuata sheria na kanuni za uchaguzi za nchi kwa kuwa zimetoa taratibu za kufuatwa katika shughuli za uchaguzi na kampeni zilitakiwa kuisha Februari 16, mwaka huu na Februari 17, mwaka huu ilikuwa tarehe ya uchaguzi.

Alidai washtakiwa wote tisa na wengine 12 ambao hawako mahakamani walikula njama kushawishi wananchi kufanya mkusanyiko usio halali, kuinua hisia za chuki kwa Watanzania na kuleta chuki na dharau dhidi ya utawala halali wa serikali halali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Washtakiwa kwa nyakati tofauti walidai kuwa hawawezi kujibu chochote mpaka uwapo wa wakili wao.

Habari Kubwa