Korti yamwonya Wema, arejeshewa dhamana

25Jun 2019
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Korti yamwonya Wema, arejeshewa dhamana

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imemwonya  msanii wa filamu nchini, Wema Sepetu, kuacha kuidharau anapokuwa na udhuru badala yake amtumie mdhamini wake kumwakilisha mahakamani.

Msanii nyota wa filamu nchini, Wema Sepetu (kushoto), akitokea mlango wa nyuma katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam jana, baada ya kuachiwa kwa dhamana. PICHA: MIRAJI MSALA

Aidha, mahakama hiyo imesema kuanzia sasa dhamana yake inaendelea na kesi hiyo itasikilizwa ushahidi wa Jamhuri Julai 4, mwaka huu, dhidi ya tuhuma zinazomkabili za  kuchapisha video ya ngono katika ukurasa wake kwenye mtandao wa Instagram.

Amri hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Maira Kasonde,  wakati akitoa uamuzi wa kufutiwa dhamana au la katika hoja zilizowasilishwa na mawakili wa pande zote mbili.

Alisema baada ya kupitia hoja za Jamhuri kwamba Wema alifikishwa mahakamani hapo Juni 17, mwaka huu, akiwa chini ya ulinzi na kiapo cha utetezi, mahakama yake imejiridhisha kwamba alivunja masharti ya dhamana.

Alisema kiapo cha mshtakiwa kinaonyesha sababu za kushindwa kufika mahakamani kwamba alipata ugonjwa baada ya kufika viunga vya mahakama hiyo.

"Swali ni kwa nini alishindwa kuijulisha mahakama wakati alikuwa eneo la mahakama? Kutokuwapo kwako mahakamani lazima umjulishe mdhamini wako ambaye ana wajibu wa kuhakikisha unafika kusikiliza kesi yako na si wakili," alisema na kuongeza kuwa:

"Mahakama yangu inakupa onyo, mdhamini wako anatakiwa kuwajibika pale unapokuwa na udhuru wa kuja kutoa taarifa. Dhamana yako inaendelea na kesi inaendelea kusikilizwa ushahidi wa Jamhuri Julai 4, mwaka huu," alisema Hakimu Kasonde wakati akitoa uamuzi wa kumwachia kwa dhamana huru msanii huyo.

Juni 11, mwaka huu, mahakama hiyo ilitoa hati ya kukamatwa Wema baada ya kushindwa kufika mahakamani kusikiliza kesi yake.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Silvia Mintanto, kuomba hati ya kukamatwa msanii huyo.

Hata hivyo, wakili wa utetezi, Reuben Semwanza, alidai kuwa mshtakiwa alifika mahakamani kusikiliza kesi yake lakini alipatwa na ugonjwa wa gafla.

Juni 17, mwaka huu, mahakama iliamuru mshtakiwa huyo kwenda mahabusu hadi jana alipoachiwa kuendelea na dhamana.

Katika kesi ya msingi, Wema (30), anadaiwa kuwa Oktoba 15, 2018 katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, alichapisha video ya ngono na kuisambaza katika mtandaoni wake wa kijamii wa Instagram.

Habari Kubwa