Korti yatoa hati kukamatwa Wema

12Jun 2019
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Korti yatoa hati kukamatwa Wema

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imetoa hati ya kukamatwa Msanii wa Filamu nchini, Wema Sepetu (30), anayekabiliwa na mashtaka ya kuchapisha video ya ngono katika ukurasa wake kwenye mtandao wa Instagram, baada ya kushindwa kufika mahakamani kusikiliza kesi yake.

Msanii wa Filamu nchini, Wema Sepetu.

Amri hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi, Maira Kasonde, baada ya upande wa Jamhuri kudai kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kusikilizwa ushahidi wa Jamhuri, lakini mshtakiwa hakuwapo mahakamani.

Wakili wa Serikali Silvia Mitanto, alidai kuwa kwa sababu mshtakiwa ameshindwa kufika mahakamani, upande wa Jamhuri unaomba hati ya kukamatwa mshtakiwa na tarehe nyingine ya kusikilizwa ushahidi.

Hata hivyo, Wakili wa utetezi, Rubern Semwanza, alidai kuwa mshtakiwa alifika mahakamani kusikiliza kesi yake, lakini alipatwa na ugonjwa wa gafla.

Hakimu alisema mshtakiwa alipaswa kufika mahakamani kujieleza udhuru wake, lakini ameshindwa kufanya hivyo mahakama inatoa hati ya kukamatwa.

Alisema mahakama yake itasikiliza ushahidi wa Jamhuri Julai 4, mwaka huu.

Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anadaiwa kuwa Oktoba 15, 2018 katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, alichapisha video ya ngono na kuisambaza katika mtandao wake wa kijamii wa Instagram.

Habari Kubwa