Korti yatupa rufani hukumu ya kunyongwa hadi kufa

26Jul 2021
Kulwa Mzee
Dar es Salaam
Nipashe
Korti yatupa rufani hukumu ya kunyongwa hadi kufa

MAHAKAMA ya Rufani imetupilia mbali maombi ya mapitio yaliyowasilishwa na Said Mapeyo, aliyehukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kosa la mauaji ya kukusudia.

Uamuzi wa mahakama hiyo ulitolewa na jopo la majaji watatu, Jaji Austine Mwarija, Jaji Mary Levira na Jaji Dk. Paul Kihwelo, baada ya kupitia sababu za mapitio na hoja zilizowasilishwa na pande zote mbili.

Mapeyo anayetakiwa kuendelea na adhabu aliyopewa, aliomba mahakama hiyo ifanye mapitio ya hukumu iliyotolewa na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani waliobariki adhabu iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam Februari mwaka 2020.

Katika maombi ya mapitio Mapeyo aliwasilisha sababu tatu za kufanya hivyo, ikiwamo kwamba hakupewa nafasi ya kusikilizwa na Mahakama ilikosea kwa kushindwa kumuita daktari aliyefanyia uchunguzi mwili wa marehemu kufika kutoa ushahidi.

Mapeyo anadaiwa kumuua Mussa Marco maarufu Mhagama, mwili wa marehemu huyo ulikutwa bila kuwa na kichwa, alishtakiwa mwaka 2017 na kuhukumiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa mwaka 2020.

Jopo baada ya kupitia hukumu hiyo, kupitia hoja za mrufani aliyejiwakilisha mwenyewe na hoja ya Wakili wa Serikali, Deborah Mushi, ilifikia uamuzi kwamba hoja zote za mapitio hazina msingi.

Mahakama ilisema kwamba sababu zilizotolewa hazina sifa ya kutolewa katika maombi ya mapitio, na kwamba Mapeyo alitaka kupitishia sababu za rufani kwa mlango wa nyuma.

"Hoja kuhusu uchunguzi wa mwili wa marehemu ni kwamba uchunguzi wa mwili ulifanyika bila kichwa, adhabu iliyotolewa ilikuwa sahihi kulingana na ushahidi uliotolewa katika mahakama hiyo ya chini.

"Katika hoja zilizowasilishwa hakuna hoja ya kuathiri hukumu ya Mahakama Kuu, maombi ya mapitio hayana msingi, Mahakama inayatupilia mbali," lilisema jopo hilo katika uamuzi wake.