Kortini shtaka la kukutwa na nyeti 5 za kike

22Jun 2022
Grace Gurisha
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kortini shtaka la kukutwa na nyeti 5 za kike

MKAZI wa Maswa, mkoani Simiyu, Salum Nkonja maarufu Emmanuel Nkonja, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka 11 likiwamo la kukutwa na sehemu za siri tano za kike na chuchu tano za wanawake.

Akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali, Carolina Matemu, alidai jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Ramadhani Rugemalira kuwa mshtakiwa alikutwa pia na nyara za serikali, yakiwamo mafuvu mawili ya binadamu na sehemu za siri za wanyama.

Matemu alidai Oktoba 30, 2017, wilayani Ubungo, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa huyo alikutwa na sikio na pembe ya nyati vyote vikiwa na thamani ya Sh. 4,318,700 bila kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Alidai kuwa, katika tarehe na eneo hilo, mshtakiwa huyo pia alikutwa na uume wa mbwamwitu wenye thamani ya Sh. 2,272,600, pamoja na uume wa nyumbu wenye thamani ya Sh. 1,477,450 bila kibali.

Ilidaiwa kuwa, Novemba 30, 2017, Wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam, mshtakiwa huyo alikutwa na mikia mitano ya ngiri yenye thamani ya Sh. 5,114,250, uume wa fisi mitatu, yenye thamani ya Sh. 3,750,450.

Pia, mshtakiwa alikutwa akimiliki yai moja la mbuni lenye thamani ya Sh. 2,827,600, ngozi moja iliyokaushwa ndege aina ya Ngekewa yenye thamani ya Sh. 227,300 na kichwa kimoja cha nyoka aina ya Kobla chenye thamani ya Sh. 193,205.

Pia mshtakiwa huyo alikutwa akimiliki viungo vya binadamu ambavyo ni sehemu za siri tano za wanawake, mafuvu mawili ya binadamu na chuchu tano za wanawake.

Mshtakiwa alikana mashtaka hayo na upande wa mashtaka ulidai, upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuomba tarehe nyingine ya kumsomea mshtakiwa hoja za awali.

Hakimu alimweleza mshtakiwa atakuwa nje kwa dhamana ikiwa atatimiza sharti la kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Shilingi milioni tano.

Hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 5, 2022 na mshtakiwa alipelekwa mahabusu kwa kukosa wadhamini.

Habari Kubwa