Kortini kufanya ugavi bila usajili

07Nov 2019
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Kortini kufanya ugavi bila usajili

WATU 18 wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, wakikabiliwa na shtaka la kufanya kazi za ununuzi na ugavi bila kusajiliwa na Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSTB).

Washtakiwa hao ni Jema Mbugi, Julieth Daniel, Jeremiah Mafuru, Lucy Wanne, Odillo Benedict, Bibiana Romanus, Bahati Wonnandi, Raphael Waryana, Joseph Mhere na Victor Kilonzo.

Wengine ni Moshi Mohamed, Avitus Rutayuga, Esther Reyemamu, Ruth Mwaipyana, Beatrice Mushi, Julieth Mwihambi, Geogre Lyimo na Estonia Kalokola

Washtakiwa hao walisomewa mashtaka yao na Mwendesha Mashtaka wa PSTB, Suleiman Mzava mbele ya Hakimu Mkazi Hudi Hudi.

Mzava alidai kuwa wanakabiliwa na shtaka la kufanya kazi za ununuzi bila kusajiliwa na bodi hiyo.

Mzava alidai kuwa kati ya Februari 11 na 15, mwaka huu katika ofisi mbalimbali jijini Dar es Salaam, washtakiwa hao walikutwa wakifanya kazi za ununuzi na ugavi bila kusajiliwa na PSTB, huku wakijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Wakati mashtaka hayo yanasomwa, washtakiwa Mehere, Mohamed, Mwaipyana na Mwihambi hawakuwapo mahakamani na upande wa Jamhuri uliomba mahakama itoe hati ya kukamatwa kwao.

Upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuomba mahakama kupanga tarehe ya washtakiwa hao kuzomewa maelezo ya awali.

Hata hivyo, washtakiwa walikana mashtaka hayo, Jamhuri haikuwa na pingamizi la dhamana.

Hakimu Hudi aliwataka washtakiwa kila mmoja kuwa na mdhamini mmoja mwenye barua kutoka Ofisi ya Serikali ya Mtaa na awe na kitambulisho cha taifa atakayetia saini hati ya dhamana ya Sh. milioni tano.

Washtakiwa waliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti na kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 21, mwaka huu, kwa ajili ya kutajwa.

Habari Kubwa