Kortini kwa kusambaza taarifa za kumdhalilisha Rais Magufuli

22Jun 2016
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Kortini kwa kusambaza taarifa za kumdhalilisha Rais Magufuli

LEONARD Kyaruzi, amefikishwa mahakamani akikabiliwa na mashtaka mawili likiwamo kuchepusha na kusambaza taarifa za kumdhalilisha Rais Dk. John Magufuli, njia ya mtandao whattsapp.

Mshtakiwa huyo alisomewa mashitaka yake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Magreth Bankika, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Wakili wa Serikali, Simon Wankyo, alidai kuwa Juni 2, mwaka huu, katika jengo la Tanzanite Tower, lililopo barabara ya Sam Nujoma, mshtakiwa alichapisha taarifa ya kumdhalilisha Rais Magufuli.

Katika shtaka la pili, ilidaiwa kuwa siku na eneo la tukio la kwanza, mshtakiwa alisambaza taarifa za kumdhalilisha Rais Magufuli kupitia mtandao wa Whattsapp.

Mshtakiwa alikana mashtaka hayo.

Hakimu Bankika alisema mshtakiwa atakuwa nje kwa dhamana kwa kuwa na mdhamini mmoja anayetambulika atakayesaini hati ya dhamana ya Sh. milioni moja.

Mshtakiwa alitimiza masharti hayo. Upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Hakimu alisema kesi hiyo itatajwa Julai 18, mwaka huu na mshtakiwa atakuwa nje kwa dhamana.

Habari Kubwa