Kortini kwa madai ya uhujumu uchumi

10Jul 2020
Hellen Mwango
Arusha
Nipashe
Kortini kwa madai ya uhujumu uchumi

WAKAZI wawili wa mkoani Arusha, Seuri Kisamu maarufu kama Mollel (34) na Losieku Mollel (35), wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, wakikabiliwa na kesi mbili tofauti za uhujumu uchumi ikiwamo kukutwa na kilo 1,378.4 za bangi.

Katika kesi ya kwanza, Kisamu amesomewa shtaka lake mbele ya Hakimu Mkazi Gwantwa Mwankuga.

Upande wa Jamhuri ulidai kuwa Juni 30, mwaka huu, katika kijiji cha Englion, Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, mshtakiwa alikutwa akisafirisha kilo 649.5 za bangi kinyume cha sheria.

Katika kesi ya pili, ilidaiwa mbele ya Hakimu Mwankuga kwamba siku ya kesi ya kwanza, mshtakiwa Losieku alikutwa akisafirisha bangi kilo 728.9 huku akijua ni kinyume cha Sheria.

Washitakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka kisheria kusikiliza kesi za uhujumu uchumi mpaka upelelezi utakapokamilika na kuhamishiwa Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Uhujumu Uchumi na Rushwa, maarufu kama Mahakama ya Mafisadi.

Hakimu Mwankuga alisema kesi hiyo itatajwa Julai 22, mwaka huu, na washtakiwa wapelekwe mahabusu.

Habari Kubwa