Kortini kwa tuhuma kujipatia 850,000/-

13Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Kortini kwa tuhuma kujipatia 850,000/-

MKAZI wa Tabata, Fortunatus Chacha, amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala akikabiliwa na shtaka la wizi wa Sh. 850,000.

Mshtakiwa huyo alisomewa shtaka hilo juzi mbele ya Hakimu Mkazi Samuel  Obasi na Mwendesha Mashtaka Grace Mwanga.

Mwanga  alidai kuwa mshtakiwa huyo  alitenda kosa hilo mwaka jana  katika hoteli ya Best Western iliyoko mtaa wa Nkrumah, Ilala jijini Dar es Salaam na kujipatia fedha hizo mali ya Veres Tamas, mkazi wa Ilala.

Alidai kuwa mshtakiwa alitumia nondo kumtisha  Tamas ili kujipatia fedha hizo na kwamba kufanya hivyo ni kosa kwa mujibu wa sheria.

Mshtakiwa baada ya kusomewa shtaka hilo, alikana na kurejeshwa rumande hadi  kesho kesi itakapotajwa.

Wakati huo huo,  Lazaro Zabron (29) mkazi wa Tabata Kimanga jijini Dar es  Salaam, alifikishwa katika mahakama hiyo kwa tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya aina ya bangi.

Akisoma shitaka hilo mbele ya Hakimu Mkazi Obasi, Mwanga  alidai kuwa Novemba 18, mwaka jana, katika eneo Tabata Kimanga, mshtakiwa  alikutwa na kete 18 za dawa hizo.

Mshtakiwa alikana shtaka hilo na kurejeshwa rumande baada ya kushindwa kutimiza  masharti ya dhamana.

Katika masharti hayo, Hakimu alimtaka mshtakiwa kuwa na wadhamini  wawili na kutia saini bondi ya Sh. milioni tano kila mmoja.

Habari Kubwa