Kortini madai kurusha maudhui bila leseni

19Sep 2020
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Kortini madai kurusha maudhui bila leseni

WATU wawili, akiwamo mwanafunzi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Isaya Massawe (22), wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na kesi mbili tofauti za kuchapisha maudhui mtandaoni bila kuwa na leseni.

Katika kesi ya kwanza, Massawe alisomewa shtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Yusto Ruboroga, aliyepangiwa kusikiliza kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

Wakili wa Serikali Adolf Ulaya alidai kuwa kati ya Februari 4, mwaka jana na Septemba 16, mwaka huu, mahali tofauti jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alitenda kosa hilo.

Ilidaiwa kuwa mshtakiwa huyo alichapisha maudhui mtandaoni kupitia channel ya YouTube yenye jina la Isaya Thomas Massawe, bila kuwa na leseni kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Mshitakiwa baada ya kusomewa shitaka hilo, alikana na upande wa mashitaka ulidai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Hakimu Ruboroga, alimtaka mshtakiwa kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili waaminifu watakaotia saini dhamana ya Sh. milioni tatu kila mmoja.

Mshitakiwa alitimiza masharti ya dhamana na yuko. kesi itatajwa Oktoba 15, mwaka huu.

Katika kesi ya pili, anayedaiwa kuwa Ofisa Habari Msaidizi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA), Dominic Mgaya, alisomewa shtaka la kurusha maudhui mtandaoni bila kuwa na leseni.

Mgaya alisomewa shtaka lake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate huku Wakili wa Serikali, Adolph Ulaya, akidai kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo kati ya Oktoba 14, 2017 mpaka Septemba Mosi, mwaka huu, jijini Dar es Salaam.

Ilidaiwa kuwa mshtakiwa alirusha maudhui hayo kupitia chaneli ya Youtube iitwayo Chadema Media TV bia kuwa na leseni kutoka TCRA.

Baada ya kusomewa shitaka hilo, mshtakiwa huyo alikana, upande wa mashtaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa ambapo ilipangwa Oktoba 20, mwaka huu.

Mshtakiwa huyo aliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza sharti la kuwa na wadhamini waliotia saini bondi ya Sh. 500,000 kila mmoja.

Habari Kubwa