Kortini madai ya kukutwa na tausi

08Aug 2020
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Kortini madai ya kukutwa na tausi

RAIA sita wa China wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, ikiwamo kuongoza genge la uhalifu na kukutwa na nyara za serikali ndege aina ya tausi isivyo halali.

Washtakiwa hao ni wafanyabiashara Jin Erhao (35), Chengfa Yang (49), Ren Yuangqing (55) Mkurugenzi wa Kampuni ya Usafirishaji ya Sinota, Shu Nan (50), mfanyakazi katika kampuni hiyo, Chen Shinguang (45) ambaye ni meneja wa kampuni hiyo na Meneja Ufundi wa kampuni hiyo, Gu Jugen (57).

Mapema juzi, washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Richard Kabate.

Upande wa Jamhuri uliongozwa na mawakili wa serikali, Salim Msemo na Elia Athanas na utetezi uliongozwa na Wakili Ibrahim Bendera.

Wakili Msemo alidai kuwa katika shtaka la kwanza, washtakiwa wanadaiwa kuongoza genge la uhalifu na kwamba Agosti Mosi, mwaka huu, mtaa wa Sokoine, jijini Dar es Salaam, wote kwa pamoja na kwa makusudi walisimamia genge la uhalifu lililosababisha kupatikana kwa tausi mmoja mwenye thamani ya dola za Marekani 500 sawa na Sh. 1,155,000 za Tanzania kinyume cha Sheria ya Wanyamapori.

Katika shtaka la pili, ilidaiwa kuwa Agosti Mosi, mwaka huu, mtaa wa Sokoine, washtakiwa hao walikutwa na tausi mmoja mwenye thamani ya Sh. 1,155,000 kinyume cha Sheria ya Wanyamapori.

Aliendelea kudai kuwa katika shtaka la tatu, washtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka la kukutwa na nyara za serikali ambayo ni tausi mmoja mwenye thamani ya Sh. 1,155,000 kosa wanalodaiwa kulitenda Agosti Mosi, katika mtaa wa Sokoine, jijini Dar es Salaam.

Baada ya kuwasomea mashtaka, Wakili Msemo alidai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na upande wa Jamhuri haukuwa na pingamizi la dhamana, lakini waliomba masharti yawe makali kulingana na mashtaka yalivyo.

Akitoa masharti ya dhamana, Hakimu Kabate aliwataka washtakiwa hao kila mmoja kupeleka wadhamini wawili wa kuaminika walio ndani ya Mamlaka ya Mahakama (ndani ya mkoa wa Dar es Salaam na Pwani) watakatiaosaini bondi ya Sh. 500,000 kila mmoja.

Pia aliwataka kuwasilisha pasi zao za kusafiria mahakamani na kutakiwa kutokusafiri nje ya mkoa wa Dar es Salaam bila ruhusa ya mahakama.

Wakili wa utetezi, Bendera, alidai kuwa pasi za kusafiria za washtakiwa hao kwa sasa zinashikiliwa na polisi, hivyo uwezekano wa kuziwasilisha kwa wakati haukuwapo. Hakimu Kabate alimtaka kuwasilisha uthibitisho iwapo ni kweli pasi hizo ziko mikononi mwa polisi.

Aliwataka mawakili wa pande zote kushirikiana kupata uthibitisho huo ili kuwapatia washtakiwa dhamana.

"Wakili Msemo mnaweza kushirikiana kupata uthibitisho hata kwa simu. Mimi nipo mkipata uthibitisho tutakamilisha dhamana, lakini kwa sasa washtakiwa watabaki mahabusu mpaka tupate uthibitisho," alisema Hakimu Kabate.

Washtakiwa walirudishwa mahabusu na kesi hiyo iliahirishwa hadi Agosti 20, mwaka huu itakapotajwa.

Habari Kubwa