Kortini tuhuma kumtumia Waziri Mkuu kutakatisha

15Feb 2020
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Kortini tuhuma kumtumia Waziri Mkuu kutakatisha

WATU watatu wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, ikiwamo kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha Sh. milioni 22.9 kwa kutumia jina la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Washtakiwa hao ni mkazi wa Kigamboni, Bahati Malila, mkazi wa Oysterbay, Regina Mambai na mkazi wa Mbezi Jogoo, Godfrey Mtonyi.

Mapema jana, watatu hao kwa pamoja walisomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mfawidhi Godfrey Isaya.
Upande wa Jamhuri uliongozwa na Mawakili wa Serikali Waandamizi, Wankyo Simon na Mkunde Mshanga.

Katika shtaka la kwanza washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuongoza genge la uhalifu katika tarehe tofauti kati ya Januari 3 na 31 mwaka huu jijini Dar es Salaam kufanya uhalifu.

Katika shtaka la pili ilidaiwa kuwa Januari 14 mwaka huu, washtakiwa wote kwa pamoja kwa nia ya udanganyifu, walishirikiana kutengeneza cheti cha utambuzi wa msaada kwamba kimetolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, huku wakijua si kweli.

Mshanga alidai kuwa katika shtaka la tatu, Januari 14 mwaka huu, washtakiwa hao walighushi cheti cha utambuzi wa msaada kikionyesha kuwa ni cheti halali kutoka kwa Waziri Mkuu, jambo ambalo si la kweli.

Upande huo wa Jamhuri ulidaiwa kuwa katika shtaka la nne, washtakiwa wote kwa pamoja walishirikiana kwa makusudi kutoa cheti cha uongo kwa Guanhui Su Biaolin Tang kilichoonyesha kuwa ni cheti halali kutoka kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, huku wakijua si kweli.

Wankyo alidai kuwa katika shtaka la tano, washtakiwa wanakabiliwa na shtaka la kuwasilisha nyaraka za uongo ambapo mnamo Januari 14 mwaka huu, waliwasilisha cheti cha utambuzi wa msaada kilichoonesha kuwa ni halali kutoka kwa Waziri Mkuu huku wakijua kuwa si kweli.

Katika shtaka la sita, washtakiwa hao wanadaiwa kujipatia fedha zaidi ya Sh. milioni 22.9 kutoka kwa Guanhui Su Tang kwa njia ya udanganyifu wakijidai kuwa ni msaada wanaopeleka kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Shtaka la saba linalowakabili washtakiwa hao ni utakatishaji pesa ambapo inadaiwa kuwa mnamo Januari 14 mwaka huu, washtakiwa walijipatia zaidi ya Sh. milioni 22.9 kwa njia ya udanganyifu huku wakijua ni zao la makosa tangulizi.

Washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi mpaka upelelezi utakapokamilika na Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) atakapotoa kibali.

Hakimu Isaya alisema kesi hiyo itatajwa Februari 28 mwaka huu na washtakiwa warudishwe mahabusu.

Habari Kubwa