Kortini tuhuma mauaji ya mke

06Jul 2019
Happy Severine
MASWA
Nipashe
Kortini tuhuma mauaji ya mke

MKAZI wa Mtaa wa Majengo katika mji wa Maswa mkoani Simiyu, Emanuel Nyandu (35), amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Maswa kwa tuhuma za mauaji ya Mkewe, Julieth Josephat (30) aliyekuwa mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Shanwa Seminari, wilayani hapa.

Akisomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Fredrick Lukuna na Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Inspekta Nassib Sweddy,  ilidaiwa kuwa Nyandu alifanya mauaji hayo Julai 2, mwaka huu saa 9:00 mchana wakiwa katika nyumba yao waliyokuwa wakiishi kama wanandoa.

Sweddy alidai kuwa mshitakiwa ambaye alikuwa na ugomvi na mkewe, alimchoma kwa kutumia kitu chenye ncha kali kichwani mara tano, shingoni mara mbili, tumboni mara nne na kisha kumpiga kwa nyundo kichwani na kumsababishia kifo.

Alidai kuwa wakati mshtakiwa akifanya mauaji hayo, hakukuwa na mtu mwingine katika nyumba yao licha ya kuishi wakiwa na  mtoto wao mdogo na binti ambaye alikuwa akifanya kazi za ndani,  ambao hawakuwapo wakati tukio hilo likitokea.

Mwendesha mashitaka huyo alidai kuwa kitendo hicho cha mauaji ni kinyume cha   kifungu cha 196 na 197 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 iliyorejewa  mwaka 2002.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, mshtakiwa hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji isipokuwa kwa kibali maalum.

Hakimu Lukuna aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 17, mwaka huu, itakapotajwa tena hivyo mshtakiwa alipelekwa mahabusu kwa kuwa kosa hilo kisheria halina dhamana.