Kubenea amwaga machozi akiachiwa kwa dhamana

12Sep 2020
Na Waandishi Wetu
Arusha
Nipashe
Kubenea amwaga machozi akiachiwa kwa dhamana

MGOMBEA Ubunge wa Kinondoni (ACT-Wazalendo), Saed Kubenea, ameachiwa kwa dhamana baada ya kudhaminiwa kwa Sh. milioni 14.5 mbele ya Hakimu Martha Mahumbuga katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.

Kubenea aliachiwa jana baada ya kudhaminiwa na wadhamini wawili ambao ni Mwenyekiti wa Wilaya wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Ephata Nanyaro na Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Mkoa wa Arusha, Mwahija Choga.

Hakimu Mahumbuga alisema mshtakiwa ametimiza masharti ya dhamana aliyotakiwa kuyafuata ikiwa ni pamoja na kulipa Sh. milioni 14.5 na kuwa na wadhamini wenye mali isiyohamishika.

“Hivyo, mshitakiwa huyu atakuwa nje kwa dhamana hadi Septemba 21 mwaka huu, kesi hii itakapotajwa tena,” alisema.

Kabla ya mshtakiwa kudhaminiwa, Wakili wake, Sheck Mfinanga, akishirikiana na Wakili Alute Munghwai, waliwasilisha mahakamani hapo vielelezo vya dhamana hiyo zikiwamo nakala za malipo ya fedha hizo, barua za utambulisho toka serikali za mtaa za wadhamini wake na kukubaliwa na upande wa mawakili wa serikali.

Septemba 7, mwaka huu, Kubenea alisomewa mashtaka yake na Wakili wa Serikali Innocent Njau mbele ya Hakimu Mahumbuga kwa kuingia nchini kinyume cha kifungu cha 45(1)(i) na (2) cha Sheria ya Uhamiaji Sura ya 54.

Ilidaiwa mahakamani huko kuwa Kubenea alikamatwa mpakani Namanga Mkoa wa Arusha Septemba 5, mwaka huu na baada ya kupekuliwa alikutwa na fedha za kigeni.

AMWAGA MACHOZI

Nje ya mahakama, Kubenea akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuachiwa huku akitokwa na machozi, aliwashukuru wananchi wa Mkoa wa Arusha na waandishi wa habari kwa kufuatilia shauri lake hatua kwa hatua tangu akamatwe Septemba 5, mwaka huu.

Katika hatua nyingine, Chama Cha ACT-Wazalendo kimesema kitaendelea na kampeni za mgombea wake huyo zilizosimama kutokana na kukamatwa na polisi kwa tuhuma za utakatishaji fedha na kuingia nchini kinyume cha sheria.

“Chama cha ACT-Wazalendo kinapenda kuutaraifu umma wa Watanzania na wananchi wa Kinondoni kwamba mgombea wetu wa ubunge, Ndugu Saed Ahmed Kubenea amepata dhamana ya Hakimu Mkazi Arusha leo (jana)," ilielezwa katika taarifa hiyo iliyosisitiza chama hicho kuendelea na kampeni kwenye jimbo hilo.

*Imeandikwa na Cynthia Mwilolezi (ARUSHA) na Enock Charles (DAR)

Habari Kubwa