Kufuru ya posho ATCL

25Jul 2021
Sanula Athanas
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Kufuru ya posho ATCL
  • Wafanyakazi walipana mabilioni kinyume cha Sheria.....

NDANI ya Ukumbi wa Bunge wanasiasa kwa miaka mingi wamekuwa wakisikika wakimwita njiwa, sasa bado wanamwita njiwa na wajao huenda wataendelea kumwita hivyo hivyo.

Ni jina ambalo wabunge wamelibatiza Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), watunga sheria hao wakigawanyika katika makundi mawili ya wanaotaka shirika liendelezwe na upande wa pili ni wa wanaodai lifutwe.

Shida ni nini? Chimbuko la mjadala ni shirika kuendeshwa kwa hasara ya mabilioni ya shilingi tangu zama za uongozi wa Rais Ali Hassan Mwinyi, sasa likiripotiwa kutengeneza hasara ya Sh. bilioni 472.853 huku watumishi wake wakilipana posho za mabilioni kinyume cha sheria.

Haiba ya kiwango hicho cha hasara kilichotajwa inatisha, lakini kiulizo kinajitokeza tena; nini mzizi wa tatizo, imekuwaje kufikia kiwango hicho na kama kuna lawama, inauangukia upande upi na kwa vipi?

Inaenda mbali kwamba mzigo huo wa hasara na udhibiti wake unakabiliwa kwa namna gani?

Ni maswali yasiyohitaji majibu ya kukurupuka, bali tafakuri ya kina na busara iliyotukuka, kutathmini undani na hatima ya mustakabali uliokwishafikiwa na shirika liendako, ili kuendelea kulishuhudia likisimama katika mazingira chanya kwa manufaa ya nchi.

Imeshatimu miezi miwili na wiki kadhaa tangu Rais Samia Suluhu Hassan alipolihutubia Bunge jijini Dodoma na kuweka wazi ATCL itabaki kuwa mali ya umma, pia kwa manufaa ya umma.

Hata kabla yake, Mkuu wa Shughuli za Serikali Bungeni, Kassim Majaliwa, alidokeza azma ya kiserikali kuendeleza maboresho ya ATCL kwa kuipanulia mtaji.

Majaliwa ambaye pia ni Waziri Mkuu nchini, alibainisha kwamba hilo linafanyika sambamba na ununuzi wa ndege mpya zikiwamo tatu ambazo mustakabali wa malipo tayari uko katika bajeti ya sasa.

Hoja ya kuwa na ATCL endelevu pia imepata ushawishi wa kumuunga mkono Waziri Mkuu Majaliwa, ingawaje kuna kundi dogo lingine la wabunge halikubaliani nayo kwa madai shirika halihitajiki tena.

Kundi dogo hilo linaundwa na wabunge kutoka vyama vya upinzani na wachache kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambao msingi wa hoja yao umezama kwenye dhana kwamba ununuzi wa ndege ya kufufua ATCL ni sawa na kuwekeza kwenye maendeleo ya vitu badala ya maendeleo ya watu.

Je, ATCL ya leo inayobeba mjadala, msukosuko wake huo umeanzia wapi? Shirika hilo ambalo awali liliitwa ATC, lilizaliwa mwaka 1977 kutokana na kuvunjika kwa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambayo moja ya taasisi zake tanzu ni lililokuwa Shirika la Ndege la Afrika Mashariki (EAA).

Ndani ya mgawanyo wa mali za EAC, kupitia mali za EAA, ndipo ikazaliwa ATC.

Hata hivyo, mgawanyo rasmi kisheria wa mali za EAC ulifanyika wastani wa mwaka mmoja tangu kuzaliwa kwa ATC.

Mwanzoni ATC ilianza kazi ikiwa na ndege moja ya kwake, sambamba na nyingine za kukodi. Ilipofika wakati wa mgawo, ATC iliambulia ndege moja aina ya Twin Otters yenye uwezo wa kubeba abiria 19.

Ndani ya muda mfupi, mwishoni mwa mwaka 1978, ATC ilipiga hatua kubwa kwa kununua ndege mbili mpya aina ya Boeing 737 zenye uwezo wa kubeba abiria 103 kila moja.

Zikiwa zimeng'arisha sifa ya nchi, pia shirika lenyewe, ndege hizo mpya zilipewa majina ya Kilimanjaro na Serengeti, viashiria vilivyoonyeshwa kwenye alama zake za mkia.

Mwaka 1980, ATC ilijitanua zaidi kwa kununua ndege nne aina ya Fokker Friendship, zenye uwezo wa kubeba abiria 44 kila moja.

Ni hatua iliyozidi kuivumisha ATC, iliyoendana na kuwapeleka mafunzoni Uholanzi wahitimu wapya wa elimu ya sekondari kwa ajili ya ufundi na urubani.

Ulikuwa mwaka wa ATC kujitanua, kwani mwaka huo huo (1980) ilinunua ndege nne aina ya Twin Otters zenye uwezo kama ile iliyotajwa awali.

ZAMA ZA MWINYI

1985 ni mwaka ulioandika historia mpya kitaifa, kustaafu kwa Mwalimu Julius Nyerere, aliyeshika usukani tangu uhuru na taifa, hali kadhalika mfumo hodhi wa siasa na uchumi tangu mwaka 1964, vyote vilikabiliwa na mabadiliko.

Ikawa ni zama mpya, Tanzania chini ya Rais Mwinyi, siasa na uchumi wa nchi nazo kuhamia kwenye mfumo huria, ambao matokeo yake kwa ujumla yalishuhudia mabadiliko makubwa kitaifa na baadhi ya maeneo hayakubaki salama.

Kwa kuwa uchumi wa nchi uliingia katika mfumo mpya, uzoefu, uwekezaji na kutomudu ushindani ni miongoni mwa mambo yaliyosababisha maporomoko makubwa katika maeneo husika, ATC na taasisi zingine za umma zilitikisika.

Mpasuko huo ndiyo Rais Mwinyi, maarufu Mzee Rukhsa, jina alilobatizwa kutokana na itikadi yake ya kiuchumi wakati huo, anakiri iliiweka njiapanda ATC na baadhi ya mifumo mingine ya kiuchumi.

Rais Mwinyi anasimulia mkasa wa ATC kwamba kuanzia waamuzi wa kiserikali - wabunge waliitaka serikali yake ipunguze matumizi yasiyo ya lazima.

Anasema alilazimika kuchukua uamuzi mgumu ukiwamo wa kutowaajiri wahitimu wote wa vyuo vikuu, suala lililokuwa geni wakati huo, kwani wahitimu wote walikuwa wanaajiriwa moja kwa moja.

Anasimulia namna rungu la uamuzi mgumu lilivyowadondokea watumishi 310 wa ATC ambao alilazimika "kuwafuta kazi" ili kupunguza mzigo wa malipo ya ujira wao.

Rais Mwinyi anabainisha hayo kwenye kitabu chake cha 'Mzee Rukhsa, Safari ya Maisha Yangu', akikiri ATC ilikuwa inasuasua, hata ofisi zake sita ndani na nje ya nchi zikafungwa.

Anasema ni zama ambazo ATC na mashirika mengine ya umma yalizalisha hasara ya Sh. bilioni 46 katika mwaka mmoja pekee (1992/93).

Anafafanua: "Ukaguzi wa mashirika ya umma wa mwaka 1992/93 uliofanywa na Shirika la Ukaguzi Tanzania, ulionesha kuwa miongoni mwa mashirika 345 yaliyokaguliwa, yalikuwapo machache yaliyopata faida ya Sh. bilioni 51.2 kabla ya kodi, lakini mengi (ikiwamo ATC) ni yale yaliyopata hasara ya jumla ya Sh. bilioni 97.2.

"Kwa maneno mengine, kwa ujumla wao waliitia serikali hasara ya Sh. bilioni 46 kwa mwaka mmoja tu kwa thamani ya fedha ya wakati huo."  

ATCL YA SAMIA

Rais Samia naye anakiri ATCL ya sasa bado inaogelea kwenye dimbwi la hasara ingawa dira yake ya kiuongozi ni kwamba inahitaji uwekezaji mkubwa, kulelewa na safari ya neema iendapo bado ipo.

Akilihutubia Bunge jijini Dodoma Aprili 22 mwaka huu, Rais Samia aliahidi kulinusuru shirika hilo, akisisitiza serikali yake haitakuwa tayari kuliona linaendelea kutengeneza hasara.

Alisema mikakati yake inajumuisha kuliwezesha kwa rasilimali ili liendeshwe kwa weledi na stadi za kibiashara zitakazohimili mikiki ya soko, huku akikiri biashara ya usafiri wa anga ni ngumu.

"Shirika limekuwa likijiendesha kwa hasara, lakini hii ni kwa sababu lilirithi madeni makubwa. Hivyo, serikali inabidi kuweka mikakati ya kulipeleka mbele," alisema.

Rais Samia pia alitaja mkakati anaoufanyia kazi unajumuisha nafuu ya kodi katika baadhi ya maeneo, hali kadhalika namna ya kuipa ATCL nafuu ya mzigo wa kodi iliyonao.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, aina ya ndege zilizoko njiani kufika nchini ndani ya mwaka wa fedha uliopo, mbili kubwa aina ya Airbus. Hata hivyo, hakutaja uwezo wake.

Ndege ya tatu ni aina ya Dash 8-Q400 De-Havilland, zote zitakapotua nchini zitaifanya serikali kuwa na jumla ya ndege mpya 12 ambazo zinatumiwa na ATCL.

Hadi sasa shirika hilo katika maboresho yake mapya lina safari za kwenda katika baadhi ya nchi ambako Tanzania ina uhusiano wa karibu zikiwamo China na India.

KUTOKA KWA CAG

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2019/20, inataja serikali ilitumia jumla ya Sh. trilioni 1.028 kununua ndege nane kati ya tisa zilizonunuliwa awali.

Vilevile, CAG Charles Kichere, anabainisha ndani ya miaka mitano ya ATCL, kati ya 2015/16 na 2019/20, shirika lilipatiwa ruzuku ya Sh. bilioni 153.711.

CAG anasema ndani ya kipindi hicho, ATCL ilipata hasara ya Sh. bilioni 153.542; huku ndani ya mwaka mmoja wa fedha (2019/20), ikipata hasara ya Sh. bilioni 60.246.

Vivyo hivyo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu huyo anasema katika mwaka wa fedha 2018/19, mapato ghafi ya ATCL yalikuwa Sh. bilioni 112; na katika mwaka uliofuata, yaliongezeka na kufika Sh. bilioni 158, ikiwa ni ongezeko la Sh. bilioni 46, ambayo ni ziada ya asilimia 41.

Haiba nzuri ya kuongezeka mapato ya ATCL, kwa upande wa pili ilichafuliwa na ongezeko la matumizi yake kutoka Sh. bilioni 134 mwaka 2018/19 hadi Sh. bilioni 193 mwaka uliofuata. Ni ziada ya matumizi Sh. bilioni 59 au asilimia 45.

Hapo kuna maana gani? Katika mwaka wa fedha 2018/19, wakati wa matumizi ya juu kwa Sh. bilioni 134, ATCL iliambulia mapato ya Sh. bilioni 112, ikiangukia hasara ya Sh. bilioni 22.

Hali kadhalika, mwaka uliofuata (2019/20) matumizi yalikuwa Sh. bilioni 193 wakati mapato yaligota kwenye Sh. bilioni 158, ukawa ni mwaka mwingine wa hasara ya Sh. bilioni 35.

Yote hayo kwa ujumla yakaifanya ATCL katika miaka hiyo miwili kupata hasara ya jumla ya Sh. bilioni 57.

KUFURU YA POSHO

CAG Kichere anabainisha kuwa Kifungu cha 7(3) cha Sheria ya Mapato ya Mwaka 2014 kiliondoa posho za nyumba, usafiri, madaraka, kufanya kazi saa za ziada, kufanya kazi katika mazingira magumu na honoraria kwa mtumishi wa serikali au taasisi ambayo bajeti yake hulipwa yote au kwa kiwango kikubwa  na ruzuku za serikali.

Hata hivyo, CAG anasema alibaini kuwa katika mwaka fedha 2019/20, ATCL ililipa jumla ya posho za Sh. bilioni 1.11 na kwamba posho hizo zililipwa bila kutoza kodi ya mapato.

Uhalisia wake ni sawa na wastani wa posho ya Sh. milioni 1.93 kwa kila mtumishi wa ATCL kwa mwaka. Ripoti ya CAG inabainisha shirika lina watumishi 575.

"Nilibaini kutokata kodi ya mapato katika posho hizo kulisababishwa na kutokuwa na ujuzi wa kutosha juu ya matumizi ya Sheria ya Kodi ya Mapato kwa watumishi ambao wanashughulika na posho na malipo ya mishahara. Hii inapelekea serikali kupoteza mapato na ATCL inaweza kupata adhabu na riba zisizo za lazima kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)," abainisha.

Kwa mujibu wa CAG Kichere, hadi kufikia mwaka huo wa ukaguzi (2019/20), ATCL ilikuwa na mtaji hasi wa Sh. bilioni 472.853.

Katika mtazamo huo wa matumizi, CAG ana angalizo la baadhi ya maeneo kwamba ni sehemu ya mzizi wa gharama kubwa unaoishia kwenye lalamiko kuu la hasara na madeni.

Mosi; anataja gharama za usafirishaji mizigo na abiria ziko juu kuliko mapato yake.

Pili; gharama ziliangukia kwenye matumizi ya kiutawala ikiwamo malipo ya stahiki za wafanyakazi yasiyoendana na kanuni na miongozo rasmi.

"Ni maoni yangu kuwa bila kudhibiti gharama za uendeshaji pamoja na za kibiashara, kampuni (ATCL) itaendelea kupata hasara," anahitimisha CAG Kichere.

HOJA ZA ATCL

Siku mbili baada ya Rais Samia kutoa angalizo lake bungeni kuhusu ATCL, mnamo Aprili 24, mwaka huu, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, akakutana na uongozi wa shirika hilo kutaka ufafanuzi.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Albinus Manumbu, anajitetea dhidi ya hoja hizo akiwa na angalizo la mambo mawili, ambayo yako nje ya uwezo wao.

"Hizi ndege ambazo ATCL inaziendesha, ni mali ya serikali na anayezimiliki ni Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA). Shirika linawajibika kulipa kodi, jambo ambalo ni mojawapo ya gharama za uendeshaji," anasema.

Manumbu pia anataja maudhui ya mkataba uliopo kati ya ATCL na TGFA siyo rafiki kwa shirika hilo la ndege kuelemewa na mzigo wa gharama.

Anatoa mfano kati ya Machi na Juni mwaka jana, Tanzania na kwingineko duniani wameumia kiuchumi kutokana na janga la corona, bado ATCL iliendelea kulipa kodi za ukodishaji ndege, ilhali haikuwa ikizalisha kibiashara.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu huyo anaongeza kwamba kuwapo riba ya Sh. bilioni 16 itokanayo na madeni endelevu tangu shirika hilo kuzaliwa, sambamba na gharama kubwa za kesi zinazoihusu taasisi hiyo, kumekuwa kukiwaumiza.

Naibu Waziri Waitara amejumuisha hoja hizo kwa kuiagiza menejimenti ya ATCL kurekebisha dosari, ili kuweka mazingira sahihi ya kutekeleza ahadi ya Rais Samia, kuchukua hatua za maboresho.

WANENAVYO WADAU

Halima Mdee, Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA), anarejea ripoti mbili zilizotolewa na CAG Ludovick Utouh na CAG Profesa Mussa Assad, zote zikiwa na maoni kwamba ATCL itangazwe kuwa mfilisi ili kuepuka madeni iliyonayo.

Utouh alikuwa CAG kwa miaka minane kuanzia 2006 hadi 2014 alipokabidhi kiti kwa Profesa Assad aliyeendelea nacho hadi Novemba 3, 2019.

Katika hoja yake, Mdee aliyekuwa Waziri Kivuli wa Fedha na Mipango, katika Bunge la 11, anafafanua kuwa hasara inayolalamikiwa sasa ATCL, ni matokeo ya kutofanyiwa kazi kwa ushauri wa CAG Utouh na Profesa Assad.

"CAG Utouh alitoa mapendekezo 15 kuepuka hasara ATCL, serikali iliyapuuza. Profesa Assad katika mwaka wake wa kwanza wa uongozi kwenye ofisi hiyo, alitoa ripoti iliyobainisha ATCL ilikuwa imetengeneza hasara kwa miaka 10 mfululizo na akatoa mapendekezo mazuri, yakapuuzwa.

"Sasa CAG Kichere anasema shirika limetengeneza hasara ya Sh. bilioni 472, tulipaswa kumtangaza njiwa wetu (ATCL) kuwa mfilisi ili kuepuka haya," Mdee analalamika.

Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, anasema kinachohitajika sasa ni kufanya anachokiita uamuzi sahihi unaojumuisha kubadili muundo wa umiliki wa ATCL.

Zitto ambaye kitaaluma ni mchumi, anasema kuna haja muundo huo ubadilishwe kwa kuhusisha mashirika  ya uhifadhi na utalii kama wamiliki.

"TANAPA (Shirika la Hifadhi za Taifa) na NCAA (Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro) wamilikishwe asilimia 60 ya shirika na hivyo waondolewe katika orodha ya mashirika ya kupeleka Hazina asilimia 15 ya makusanyo yao ghafi.

"Vilevile, mashirika haya ya utalii yaachiwe kujiendesha na kukusanya mapato yao wenyewe.

"Asilimia 40 zilizobaki zimilikiwe na serikali ambapo shirika likikaa vyema, asilimia 25 ya shirika wamilikishwe wananchi kupitia Soko la Hisa la Dar es Salaam, ili kuongeza uwazi na kuboresha misingi bora ya uendeshaji wa shirika," Zitto anashauri.

Wakati serikali ikiweka mikakati kuepuka hasara, Chama cha Kimataifa cha Usafiri wa Anga (IATA) kinatahadharisha kuwa mashirika ya ndege mwaka huu yanatarajiwa kupata hasara ya jumla ya Dola za Marekani bilioni 47.7.

IATA inabainisha kuwa kiwango hicho cha hasara kinatarajiwa kuongezeka kutoka hasara ya Dola bilioni 38 iliyoripotiwa mwaka jana, sababu kubwa ikiwa ni mlipuko wa virusi vya corona.

Habari Kubwa