Kujisomea usiku chanzo mimba za utotoni

17Apr 2021
Neema Emmanuel
MWANZA
Nipashe
Kujisomea usiku chanzo mimba za utotoni

TABIA ya watoto kutoka nyumbani kwenda kujisomea usiku wamegeuza fursa ya kufanya ngono zembe na kucheza gemu huku wazazi wakiamini watoto wao wameenda kujisomea jambo ambalo linachangia kufanya vibaya na kuambulia mimba za utotoni.

Hiyo ni baada ya takwimu kutoka Jeshi la Polisi mkoani Mwanza kuonyesha makosa ya ukatili kuanzia Januari hadi Disemba mwaka jana kwa wilaya zote za mkoa wa Mwanza yalikuwa 1644 kati ya hayo mimba kwa wanafunzi zilikuwa 634, kutoroshwa wanafunzi 205,makosa yote ya ukatili 28, kubaka 250 na kulawiti 52.

Akizungumza wakati wa kikao kilichowahusisha walimu,wanafunzi, wazazi , polisi, maafisa ustawi wa jamii, viongozi wa mitaa na kata na wadau mbalimbali wa watoto, Mratibu Mradi kutoka Shirika la Kutetea Haki za Wasichana na Wanawake (KIVULINI), Eunice Mayengela,  alisema wamewakutanisha wadau hao kwa lengo la kupanga mikakati ya pamoja itakayosaidia kutokomeza mimba katika umri mdogo hususani kwa wanafunzi.

Alisema wanafunzi wengi wanatenda matendo maovu kwa kutumia mwamvuli wa kwenda kujisomea nyakati za usiku hivyo  Shirika la KIVULINI linatekeleza mradi wa “Sauti Yangu, Haki Yangu” ikilenga kutokomeza mimba katika umri mdogo katika Kata za Bugogwa, Sangabuye na Kayenze wilayani Ilemela  wanawahamasisha watoa maamuzi ili waweze kupunguza mimba kwa watoto na kutengeneza mazingira rafiki ya huduma ya afya ya uzazi kwani vitendo vinavyofanywa na watoto hao vinachangia ufahulu hafifu na uwepo wa mimba.

Alisema maofisa afya wamekuja na mbinu ya kutoa elimu katika mashule ili kuwajengea uwezo watoto hasa wa kike kuhusiana na afya ya uzazi ili waweze kutambua madhara ya mimba za utotoni , kujitambua na kufikia malengo yao pamoja na kuanzisha klabu za afya mashuleni na kuwajengea uwezo walimu ambao ni walezi ili wawe na uwezo wa kusimamia, kuziendesha na kuwanufaisha wanafunzi.

Habari Kubwa