Kukamilika Bandari ya Kabwe, kukuza biashara Kongo

13Jun 2019
Mary Geofrey
RUKWA
Nipashe
Kukamilika Bandari ya Kabwe, kukuza biashara Kongo

MKOA wa Rukwa, unatarajiwa kukuza biashara ya mazao ya chakula katika nchi za Demokrasia ya Kongo, Burundi na Zambia, kufuatia kukamilika kwa bandari ya kisasa ya Kabwe inayojengwa na Mamlaka ya Bandari (TPA) kwa Sh. bilioni 7.498.

Meneja wa Bandari ya Kigoma, Ajuaye Msese, akionyesha sehemu ya ujenzi unaondelea katika bandari ya Kabwe, Wilayani Nkasi mkoani Rukwa.

Wananchi wa mkoa huo, wamekuwa wakisafirisha mchele, mahindi, maharage, unga na sukari kwenda nchi hizo kwa kutumia mitumbwi lakini baada ya ujenzi wa bandari hiyo kukalimika watasafirisha kwa kutumia meli.

Meneja wa Bandari ya Kigoma ambaye pia anasimamia bandari zote za Ziwa Tanganyika, Ajuaye Msese, akizungumza na waandishi wa habari waliotembela bandari hiyo jana, amesema ujenzi wake umefikia asilimia 50 na unatarajiwa kukamilika Aprili 2020.

 "Kama mnavyoona bandari hii tunayojenga ya kisasa, itaenda kufungua uchumi wa wakazi wa mkoa wa Rukwa, kwa sababu wanategemea sana biashara ya kuuza mazao yao katika nchi za Congo na Burundi," amesema Msese.

Ameeleza kuwa, bandari ndogo iliyopo ina kina kifupi hivyo haiwezi kupakia mizigo mingi na ya kutosha mahitaji ya nchi hizo ndio sababu ya TPA kuanza kutekeleza mradi huo.

Msese amesema mbali na kujenga gati la kisasa lenye kina kirefu, pia wanajenga barabara na maegesho ya magari unaotekelezwa na Mkandarasi Sumry's Enterprises Ltd kwa gharama za TPA.

Amesema mradi huo pia unajumuisha jengo la kupumzikia abiria, jengo la mgahawa, ghala la kuhifadhia mizigo, nyumba za wafanyakazi na uzio.

Msese amesema mbali na miradi hiyo pia wamejenga ofisi za taasisi za Serikali katika bandari hiyo na zote nchini ili kudhibiti uingiaji wa bidhaa feki na wahamiaji haramu. Amesema mamlaka ya Bandari inafanya kazi na Mamlaka ya Mapato (TRA), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) na Shirika la Viwango Tanzania(TBS) ili kudhibiti uhalifu katika mipaka hiyo.

Habari Kubwa