Kukosekana wakalimani kwawakwaza walemavu

15Oct 2020
Christina Mwakangale
Dar es Salaam
Nipashe
Kukosekana wakalimani kwawakwaza walemavu

CHAMA cha Wakalimani wa lugha ya alama nchini, kimeeleza kuwa uchache wa wakalimani kunasababisha wenye ulemavu hususan viziwi kukosa ujumbe kwenye mikutano ya kampeni.

Billbosco Muna, mwenyekiti wa chama hicho, alisema hakuna wakalimani katika mikutano ya kampeni inayoendelea nchini, hivyo ujumbe hauwafikii watu ambao ni viziwi.

Muna aliyasema hayo katika mahojiano na kituo kimoja cha redio akizungumzia umuhimu wa wakalimani wa lugha kwa kundi la wenye ulemavu.

“Kuna idadi ndogo ya walimu wenye ujuzi wa kukalimani lugha mbalimbali, ili kumfikia mwenye ulemavu ujumbe unaotolewa hasa mikutano ya kampeni.

Kuna baadhi ya vyombo vya habari hutumia wataalamu hawa,” alisema Muna na kuongeza:

“Tunaposema ukalimani ni mchakato kutoka kwa mpokeaji yaani mkalimani aibadili lugha kwenye ubongo wake na kuufikisha ujumbe kwa lugha ya alama kwa kiziwi.”

Waziri Mkuu, Kassimu Mjalaiwa, Septemba mwaka jana, wakati akihutubia wananchi kwenye kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Viziwi Duniani, alisema mitaala ya vyuo vya afya, polisi, mahakama na vinginevyo vihakikishe vinaongeza kozi ya lugha ya alama.

Alisema lugha hiyo iwe kama somo, la lazima ili kusaidia kuzalisha watalaamu wa lugha ya alama ambao wataweza kuwahudumia viziwi ipasavyo.

“Utoaji wa elimu katika ngazi mbalimbali pamoja na kuboresha mawasiliano katika jamii na tayari imetoa mafunzo ya lugha hiyo awamu ya kwanza kwa walimu 82 wa shule za sekondari,” alisema.

Habari Kubwa