Kuku wa kisasa wazua jambo bungeni

30May 2019
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Kuku wa kisasa wazua jambo bungeni

BUNGE limeelezwa kuwa hakuna utafiti wa kisayansi ambao unaonyesha kuku wa kisasa (broilers) wana madhara kwa afya za binadamu ikiwamo kusababisha vitambi.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega

Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, alijibu swali la Mbunge wa Konde(CUF), Khatib Said Haji, kwa niaba ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.


 

Mbunge huyo alisema watu wanaotaka kupunguza mwili au vitambi wanakatazwa kula baadhi ya aina ya nyama na kushauriwa kula samaki na kuku.
“Lakini katika nyama za kuku, kuna kuku kutoka nje ambao wanauzwa, wana mapaja kama watu hao. Je, hao kuku wa kizungu hawana uhusiano wa moja kwa moja kwenye kuongeza vitambi?"

Mbunge huyo alihoji.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Ulega alisema ulaji wa kuku wa kisasa na ulaji wa kuku kwa ujumla unaongeza protini ambayo huwa inatokana na wanyama na mimea.
Alibainisha kuwa hakuna utafiti wa kisayansi uliothibitisha kuwa kuku hao wana madhara kwa binadamu.


“Ulaji wa kupitiliza ndiyo utakaoweza kusababisha hayo matatizo, lakini broilers hawana shida yoyote, kinachowafanya wakue ni homoni ambazo kisayansi ni vitamins.

Kwa hiyo, sisi wana sayansi tunachokifanya, vyakula vya broilers tunaweka vitamins za kutosheleza kuhakikisha ukuaji wao unakua ni wa haraka kulinganisha na kuku wa kienyeji," alisema.


Katika swali la nyongeza, Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Musukuma, alihoji serikali inatoa ushauri gani kwa wasio na vitambi wale vyakula gani kwa kuwa pamoja na matumizi ya vyakula vya wanga, bado wapo kwenye maumbile hayo hayo.
Akijibu swali hilo, Ulega alimshauri mbunge huyo kuwaona wataalamu wa lishe ili kumpangia vyakula vitakavyoweza kumsaidia kupata kitambi.

Awali, katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Khadija Nassir Ali, alisema uzito mkubwa mwilini ni dalili za mwanzo za magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
“Je, serikali ina mkakati gani wa kupambana na magonjwa haya? Mbali na mazoezi, ni mbinu gani nyingine za kitaalamu za kupambana na kitambi?" Mbunge huyo alihoji.


Akimjibu mbunge huyo, Ulega alisema serikali inatengeneza mpango mkakati wa mwaka 2016-2020 wa kupambana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Alisema kitambi ni dalili mojawapo ya uzito uliopita kiasi na si dalili njema na husababisha magonjwa hayo.


“Njia bora ya kupambana na kitambi ni kujikinga kutokukipata kwa kuhakikisha unazingatia ulaji wa vyakula unaofaa na ufanyaji wa mazoezi," Ulega alisema.

Habari Kubwa