Kulisha mifugo mashambani sasa kukaa mahabusu siku 10

22Feb 2021
Richard Makore
Magu
Nipashe
Kulisha mifugo mashambani sasa kukaa mahabusu siku 10

MKUU wa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, Salum Kali, ametangaza kuwakamata na kuwaweka mahabusu kwa siku 10 mfululizo kabla ya kuwafikisha mahakamani wafugaji wakorofi wanaolisha mifugo yao kwa makusudi kwenye mashamba ya wakulima.

Alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki katika kijiji cha Nyashimba katika Kata ya Nyigogo, wilayani Magu alipokutana na wafugaji na wakulima.

Alisema mfugaji  atakayekamatwa amelisha mifugo yake katika shamba la mkulima afikishwe kwake na ataagiza awekwe mahabusu kwa siku 10 mfululizo kabla ya kufikishwa mahakamani ili iwe fundisho.

Akizungumza na wakulima na wafugaji katika kijiji hicho, Kali alisema serikali inatakiwa kushughulikia kero ya madawati, barabara, zahanati, huduma za maji pamoja na umeme,  lakini siyo kusuluhisha migogoro ya wakulima na wafugaji.

Alisema kuanzia sasa mifugo itakayokamatwa shambani inauzwa na fedha hizo zitatumika kujenga zahanati, madawati na huduma za afya.

Aidha, aliwataka wakulima kuacha njia ya upana wa mita 15 ili kupitisha mifugo badala ya kulima eneo lote na kusababisha migogoro na wafugaji.

''Wote nyinyi ni ndugu, mpendane, mheshimiane kwa sababu mnaishi pamoja mnapakuliana mboga na kuombana moto, hivyo lazima muishi kwa upendo na kuacha migogoro,''  alisema  Kali.

Kali alisema ni aibu kwa uongozi ngazi ya wilaya kwenda kushughulikia masuala ya migogoro ya wakulima na wafugaji vijijini badala ya kufanya mambo makubwa ambayo yataisaidia jamii kupiga hatua.

Aidha, aliwataka wenyeviti wa vijiji na vitongoji kumaliza migogoro ya wafugaji na wakulima inayotokea katika maeneo yao badala ya kusubiri viongozi wa juu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, mkoani Mwanza, Hondola Mpandalume, aliwaonya watendaji wa kata na vijiji wanaoshindwa kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji.

Aliahidi kukutana na madiwani wa halmashauri hiyo na kutunga sheria ndogo ndogo,  lakini kali ili kuhakikisha wakulima wanaacha njia za mifugo na wafugaji hawasogei kwenye mashamba ya wakulima.

Habari Kubwa