Kunenge aagiza kukamatwa aliyehujumu ufuta,korosho

24Sep 2021
Yasmine Protace
Mkuranga
Nipashe
Kunenge aagiza kukamatwa aliyehujumu ufuta,korosho

MKUU wa Mkoa wa Pwani,Abubakari Kunenge ameagiza kukamatwa na kuchukuliwa maelezo Mkurugenzi wa Kampuni ya I&D kwa kuwahujumu wakulima wa korosho na ufuta mkoani humo.

Ramadhani alikamatwa ,akiwa katika kikao chawadau wa korosho Mkoa wa Pwani,kutokana na Mwenyekiti wa Chama Kikuu Mkoa wa Pwani,Mussa Hemed,kueleza jinsi manzao hayo yanavyohujumiwa na kusababisha wanunuzi kugoma kuunua mazao hayo yanayotunzwa katika magala ya Kimanzichana  Mkuranga.

Akisoma taarifa yake mbele ya mkuu wa mkoa wa Pwani,pamoja na wadau wa korosho,Mussa alisema kuwa  wanafanya kazi katika mazingira magumu katika msimu wa korosho kutokana na zao hilo kuhujumiwa na kusababisha  wanunuzi kutonunua mazao hayo katika wilaya ya Mkuranga hususani Kimanzichana Kusini.

"Wanunuzi hawataki kununua mazao ya Mkuranga Kimanzicha hiyo inatokana na kufanywa kwa ubadhirifu mkubwa wa mazao yakiwa katika gala,"alisema.

Musa aliongeza kuwa mkurugenzi wa kampuni ya I&D  Ramadhani ameajiri watunza magala ambao sio waaminifu.

Alisema  mkurugenzi huyo anatunza magala ya Kibiti na  Kimanzichana  ambapo Kampuni yake iliwaajiri watu kufanya kazi lakini hawakuwa waaminifu.

Aliongeza kuwa ufuta wa wakukima Kimanzichana Mkuranga iliingizwa katika gala ukiwa tani 87  ukaibiwa wote.

Alisema baada ya kuibiwa walimbana mtunza gala na hapo ndipo aliporudisha tani 59.500 na kubaki tani 28.500 ambazo thamani yake ni shilingi milioni 77.

Alisema katika gala hilohilo Kimanzichana ufuta wa wakukima tani 26 wenye thamani ya shilingi milioni 39 nao umepotea na wakulima wanadai pesa zao.