Kunenge aanzisha mpango shirikishi chanjo mkoa wa Pwani

25Sep 2021
Julieth Mkireri
PWANI
Nipashe
Kunenge aanzisha mpango shirikishi chanjo mkoa wa Pwani

SERIKALI mkoani Pwani imesema imeanzisha mpango harakishi shirikishi kuokoa maisha ya wananchi  wa Mkoa huo kwa kuwawezesha kupata chanjo ya  UVIKO-19 mahali popote walipo.

Aidha tayari wataalamu 550 wameandaliwa na watapewa mafunzo ya kutoa chanjo kwa wananchi watakaokuwa tayari kupata chanjo ya UVIKO 19

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge alipokuwa akifungua kikao cha wadau wa afya ya msingi kilichofanyika leo mjini Kibaha ambacho kimelenga kufanya tathmini na kuweka mikakati ya kuchanja wananchi wengi zaidi.

" Tulizindua utoaji wa chanjo ya UVICO 19 Julai 30 mwaka huu tukiwa na vituo 27 katika Mkoa wetu na sasa viko zaidi ya 200 lakini pia tutafika mpaka nyumbani kwa mwananchi ambaye atahitaji kupata chanjo hii atafikiwa alipo na wataalamu wetu" alisema Kunenge.

Mkuu huyo wa mkoa amesema walipokea chanjo 30,000 na hadi sasa wananchi 15,000 ndio waliochanja jambo ambalo linawafanya kuendelea kutoa Elimu zaidi ili waliobaki wajitokeze na kuokoa chanjo iliyobaki isiharibike.

" Chanjo 15,000 zilizobaki zimebakisha mwezi mmoja ziharibike hazitatumika tena baada ya muda huo wananchi wenye utayari wajitokeze wapate chanjo  kuokoa maisha yao" alisisitiza.

Mganga mkuu wa Mkoa wa Pwani Gunini Kamba amesema endapo wananchi wengi watajitokeza kupata chanjo ya UVIKO 19 matumizi ya barakoa yatapungua.

Habari Kubwa