Kura ya maoni ACT sasa kuamua Serikali ya Umoja

27Nov 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Kura ya maoni ACT sasa kuamua Serikali ya Umoja

VIONGOZI wa Chama cha ACT-Wazalendo wanaendelea na vikao vya kujadili waingie au la katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) Zanzibar, baada ya mchakato wa kukusanya maoni ya wanachama kutoka majimbo ya Unguja na Pemba kukamilika.

Vikao hivyo ambavyo vimekuwa vikifanyika kwa usiri mkubwa hata hivyo, vinadaiwa kuwagawa wanachama makundi mawili, ambapo wapo wanaunga mkono wazo la kuingia katika serikali na wengine wakipinga kwa hoja kuwa halina tofauti na msimamo uliochukuliwa baada ya  Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 pamoja na uchaguzi wa marudio wa mwaka 2016.

ACT YAFUNGUKA

Hata hivyo, alipoulizwa Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho Zanzibar, Salum Bimani, kuhusiana na suala hilo, alisema: “Chama bado kinaendelea na vikao vyake kuhusu msimamo wake wa kuingia katika serikali au laa.”

Bimani aliyasema hayo, huku taarifa za zisizo rasmi zikieleza kwamba mchakato wa viongozi wa ACT-Wazalendo wa kukutana na wanachama katika majimbo ya Unguja na Pemba ukiwa umekamilika na kazi kubwa inayofanyika hivi sasa ni kufanya uchambuzi wa maoni ya wanachama na kuangalia faida za kuingia katika serikali hiyo na hasara zake.

Akizungumza baada ya kuwaapisha mawaziri, Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, alisema ametenga nafasi mbili ikiwamo ya Waziri wa Biashara na Viwanda, na Wizara ya Afya, Maendeleo na  Jinsia kwa chama cha upinzani, ambacho kimetimiza masharti ya Katiba ya Zanzibar ya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa mgombea anayepata zaidi ya asilimia 10 ya kura za urais.

“Tumewaandikia ACT-Wazalendo kuteua jina la Makamu wa Kwanza wa Rais, lakini hadi sasa hawajaleta majibu… lakini tusiwasemee kwa sababu muda bado upo kwa mujibu wa katiba,” alisema DK. Mwinyi wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuunda Baraza la Mawaziri hivi karibuni.

Kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi, ACT- Wazalendo ina viti vya majimbo manne kwa nafasi ya uwakilishi, lakini kiti kimoja kiko wazi baada ya Mwakilishi Mteule wa Jimbo la Pandani, Abubakar Khamis Bakari, kufariki dunia kabla ya kula kiapo.

Aidha, matokeo hayo ya uchaguzi yameandika historia mpya ya kisiasa Zanzibar, baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa mara ya kwanza kuchukua majimbo yote 32 Unguja tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 na kurejesha uhai wa CCM kisiwani Pemba baada ya kushinda majimbo 14.

Iwapo Chama cha ACT kitaridhia kuingia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa, kitakuwa cha pili kujumuishwa katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa kikitanguliwa na Chama cha Wananchi (CUF) baada ya kufikiwa maridhiano kati ya Rais mstaafu wa awamu ya sita, Amani Abeid Karume na Maalim Seif Sharif Hamad kabla ya kufanyika marekebisho ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Muafaka uliozaa maridhiano ulitokana na mpasuko wa kisiasa uliojitokeza mwaka 2001 baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2000 na kusababisha zaidi ya watu 30 kupoteza maisha katika maandamano yaliyoitishwa na CUF kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu na matukio yaliokuwa yamejitokeza katika uchaguzi huo.

Habari Kubwa