Kushinda kwashindwa kuwarudisha kortini

28Nov 2016
Grace Mwakalinga
Mbeya
Nipashe
Kushinda kwashindwa kuwarudisha kortini

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe, ameagiza mahakimu 28 walioshinda kesi zilizokuwa zikiwahusisha na masuala ya mbalimbali, ikiwamo rushwa, wasirejeshwe kazini kutokana na kuweka dosari katika utendaji kazi wao.

Badala yake, Dk. Mwakyembe ameiagiza Tume ya Mahakama iwatafutie kazi nyingine.

Akizungumza jana na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Mbeya na taasisi zilizo chini ya Katiba ya Sheria, Dk. Mwakyembe alisema kuwa Tume ya Mahakama ambayo inasimamia utendaji wa mahakama, isiwarudishe tena kazini mahakimu hao kwani wananchi hawatakuwa na imani nao hasa katika masuala ya utoaji haki.

Waziri Mwakyembe yupo katika ziara ya siku tatu kwenye Mikoa ya Mbeya na Songwe.

Alisema Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga vyema kusimamia haki na sheria, hivyo Mahakama haina budi kutekeleza wajibu wake na kujenga imani kwa wananchi ili wasitilie shaka.

“Ninashauri mahakimu hao ambao walituhumiwa kwa makosa mbalimbali likiwamo la rushwa, wasirudishwe tena kwenye nyadhifa zao kwani wameshaweka dosari katika utendaji kazi wao na hata kuondoa imani kwa wananchi," alisema Dk. Mwakyembe.

"Tunataka kurudisha imani kwa wananchi wetu hasa katika chombo cha mahakama ambacho kinasimamia sheria na haki.”

Aidha, alifafanua kuwa katika suala zima la kutoa huduma ya sheria na haki kwa wananchi, kamati za maadili ambazo huanzia ngazi ya wilaya, zinatakiwa kufanya kazi kwa weledi bila kuwapo kwa kiashiria chochote cha rushwa.

Alisema kwa kufanya hivyo wananchi watapata huduma ya kuridhisha na kujenga imani kwa Mahakama kutokana na maamuzi watakayokuwa wanayatoa.

Aliongeza kuwa kama wizara yenye dhamana na masuala ya sheria na katiba, ina lengo la kuweka utawala wa sheria usiokuwa kwa kuzingatia kanuni na sheria kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

“Lengo la kufanya mambo yote haya ni kuimarisha huduma zetu za kimahakama na kumwezesha mwananchi kusaidiwa kwa wakati.

"Lakini hatuwezi kufanikisha peke yetu bila kuwa na ushirika na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi pamoja na wadau wengine.”

Habari Kubwa