Kutua ndege ya KLM Boeing 787-10 KIA, heshima kwa Tanzania

03Jul 2019
Na Mwandishi Wetu
HAI
Nipashe
Kutua ndege ya KLM Boeing 787-10 KIA, heshima kwa Tanzania
  • Imetua na watalii 334 ikielekea Dar es Salaam na Amsterdam, Uholanzi

MKUU wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya amesema hatua ya Shirika la Ndege la Kimataifa la KLM kutua kwa mara ya kwanza kwa ndege yake mpya ya Boeing 787-10 katika ardhi ya Kilimanjaro inawafunga midomo  viongozi waliozoea kuishi kama mafarisayo.

NDEGE YA SHIRIKA LA NDEGE LA KIMATAIFA LA KLM IKIWA TAKATIKA UWANJA WA NDEGE WA KIA.

Ndege hiyo ambayo ni toleo jipya la ndege ya Bombadier ilitua jana usiku katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) uliopo Wilaya ya Hai ikiwa na watalii 334 ikielekea Dar es Salaam na Amsterdam, Uholanzi.

"Hii ndio sehemu ya kwanza KLM kutua hapa Tanzania na ni nchi ya nne duniani inatua na hapa Tanzania ndiko sehemu ambayo KLM inapata faida zake, huu ni ushahidi wa wazi kabisa na hii ndio inathibitisha na inajaribu kuondoa aibu kwa maneno ya watu wengi, viongozi wengi wanajaribu kuivunjia heshima nchi hii.

"Nimewasikia wanasema kwamba nchi hii iko katika kipindi cha wasiwasi, eti kwa sababu wazungu au wageni watashindwa kuja kutokana na hali ya kiusalama na hiyo si kweli hata kidogo, labda kama ni mazingira tuliyoyazoea Watanzania na ni baadhi kwamba tumezoea kuishi mazingira ya uandishi na ufarisayo," amesema

Amesema kutua kwa ndege hiyo kubwa ya KLM ni ushahidi mwingine kuwa Tanzania kama nchi inazidi kupata heshima kubwa, inaonyesha na inathibitisha kwamba angalau bado nchii hii inaendelea kukubalika na kuaminika na diplomasia yake imekua kimataifa kutokana na mazingira yaliyoboreshwa kwa ajili ya utalii, miundo mbinu yake na usalama wa anga.

Aidha, Ole Sabaya amesema dunia nzima bado inaendelea kuiamini Tanzania kama ambavyo KLM inavyofanya wakati inakamilisha miaka 100 toka kuanzishwa kwake. Ndege hiyo ilizinduliwa wiki iliyopita na Rais wa Uholanzi katika Jiji la Amstadam.

Pia, Ole Sabaya ameonya baadhi ya viongozi, akisema ifike mahali iwe sasa basi kwa maisha ya kuhukumu kila siku kwamba katika serikali hakuna jambo lolote limefanywa na watu wengine na wao wanaona na kuamini wanastahili zaidi. 

Zaidi Mkuu huyo wa Wilaya amesisitiza kuwa: "Huu ni ushahidi kabisa kwamba nchi hii inaendelea kuaminika kimataifa na hii ni heshima tumepewa kama nchi na labda huo wasiwasi unaosemekana labda ni ule wasiwasi waliouzoea wa zamani ambapo wao kila siku ambapo wao kulikuwa na mashindano ya watanzania au viongozi kupishana juu ya anga wakitumia kodi za watanzania.

Awali akizungumza na marubani na watalii hao, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk. Anna Mghwira amesema ujio wa ndege hiyo utafungua fursa za utalii na kutengeneza mahusiano mazuri kati ya Uholanzi na Tanzania.

"Nimezungumza nao hasa hao marubani na wamenihakikishia watakuja pia na familia zao kutembelea hifadhi zetu, huyo mmoja alishapanda Mlima Kilimanjaro lakini pia KLM wametualika kwao Oktoba 19 mwaka huu, siku ambayo wanaadhimisha miaka 100 tangu kuanzishwa shirika hilo la ndege,"amesema 

Habari Kubwa