Laini za simu mil. 10 kuzimwa

15Feb 2020
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Laini za simu mil. 10 kuzimwa

MAMLAKA ya Udhibiti wa Mawasiliano (TCRA), imetangaza kuwa itazifunga laini zingine za simu zaidi ya milioni 10 zenye wamiliki takriban milioni 3.5 kutokana na kutosajiliwa kwa mfumo wa alama za vidole.

Kwa mujibu wa taarifa yao iliyotolewa jana na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA kwa vyombo vya habari, idadi ya laini ambazo hadi Jumatano zilikuwa bado hazijasajiliwa kwa mfumo huo ni 10,829,442.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa laini hizo zilisajiliwa kwa kutumia kitambulisho cha mpigakura na Mzanzibari Mkaazi.

“Uhakiki kwa kushirikiana na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) unaendelea na utaratibu wa kuzifunga unatekelezwa,” TRCA ilieleza katika taarifa yake hiyo.

Mamlaka hiyo pia ilisema idadi ya laini zilizosajiliwa kwa alama za vidole hadi Jumatano ni 32,948,073, sawa na asilimia 75.3 ya zote.

“Taarifa ya usajili hadi Jumatano ya wiki hii, jumla ya laini zote za simu zilizounganishwa mitandaoni ni 43,777,515, na laini zilizozimwa ni 7,316,445.

“Tayari watumiaji wa laini 1,790,646 wamezirudisha kwa kusajili kwa alama za vidole, hivyo kufanya idadi ya laini zilizozimwa kubakia 5,525,799,” ilifafanua.

Uzimaji wa laini za simu ambazo hazijasajiliwa ulikuwa ufanyike Desemba 31, mwaka jana, lakini Rais John Magufuli aliongeza siku 20 na mchakato huo ulikamilika Januari 20 na baada ya hapo TCRA imekuwa ikizizima kwa awamu laini ambazo hazijasajiliwa.

Habari Kubwa